Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo amefungua kikao kazi cha maandalizi ya awali ya ujumuishwaji wa afua za lishe katika mipango na bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2019/20. Mafunzo yaliyotolewa katika kikao hiki yamehudhuriwa na wakuu wa idara na taasisi za wilaya ya Mpwapwa, Wataalam wa Lishe toka OR - TAMISEMIna Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Wadau toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Wadau toka shirika la ACTION AGAINST HUNGER. Mafunzo haya yametolewa na kuwezeshwa na Serikali kupitia shirika la ACTION AGAINST HUNGER ili kufikia hatua muhimu katika uboreshaji wa shughuli za lishe Wilayani Mpwapwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (watatu kushoto) akiwa na wakuu wa idara, taasisi na wataalam wa lishe toka Mkoani Dodoma, OR TAMISEMI na Wizara ya Afya Nje ya Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mara baada ya kufungua Kikao kazi cha Kamati ya Lishe Wilaya.
Mhe. Shekimweri amesema, "Takwimu za 30/06/2018 katika zoezi la Upimaji wa Hali ya Lishe, utoaji wa dawa za minyoo na matone ya Vitamin A zimebaini kuwa utapiamlo bado ni tatizo kubwa linaloathiri watoto walio na umri chini ya miaka mitano hapa Wilayani Mpwapwa. Kwa mujibu wa takwimu; Udumavu ni asilimia 37, Uzito pungufu ni asilimia 12,Wakondefu ni asilimia 1. Hali hii ni mbaya na inahitaji nguvu kubwa ielekezwe kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto wetu ambao ndio nguvu kazi ya taifa la kesho".Wajumbe wa Kikao kazi cha Kamati ya Lishe Wilaya wakisiliza kwa makini maelekezo ya mafunzo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa
Mkuu wa Wilaya Mhe. Shekimweri katika hotuba yake amesema, ikumbukwe kuwa; mnamo tarehe 19/12/2017, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa niaba ya Makamu wa Rais alisaini Mkataba wa utekelezaji afua za lishe na Wakuu wa Mikoa yote nchini. Mkataba wenye lengo la kuchochea utekelewa shughuli za lishe kwa kasi hapa nchini utadumu kwa muda wa miaka minne (01 Januari, 2018 hadi Juni 30, 2021; na una viashiria kumi (10) ambavyo wakuu wa Mikoa wanapimwa majukumu kila baada ya miezi 6. Hivyo, natoa rai kwa watendaji wa ngazi zote na haswa kamati za lishe kutenga fedha kwenye mipango na bajeti kufuatana na miongozo yaani Tsh. 1000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano. Fedha hizi zitengwe kutoka kwenye vyanzo vinavyooaminika na usimamizi wa utekelezaji wa kila kiashiria uimarishwe zaidi. Ni matarajio yangu kuwa kila robo nipata taarifa ya utekelezaji na nataka nione matokeo yenye tija.
Sambamba na hilo Mkuu wa Wilaya ameagiza kuwa taarifa ya utekelezaji wa lishe ya kila robo mwaka iwasilishwe ofisini kwake na iwekwe katika tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, katika ziara zake Afisa Lishe na Afisa TEHAMA waambatane pamoja kwa ajili ya kutoa elimu ya lishe wa wananchi pamoja na kuzichukua taarifa hizo na kuziweka katika tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Afisa LISHE wa Wilaya ya Mpwapwa akiwasilisha shughuli za lishe zilizotekelezwa kwa Wajumbe wa Kikao kazi cha Kamati ya Lishe Wilaya katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa
Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imeazimia yafuatayo:-
1. Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa iendelee kutenga na kutoa fedha Tsh 1,000/= kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 5.
2. Afisa lishe wa wilaya apewe siku ya kutoa semina yalishe katika kila vikao vya kisheria vya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa katika ngazi zote.
3. Lishe iwe ni agenda ya kudumu katika ngazi zote za kuanzia kijiji, kata, tarafa hadi wilaya, pia taarifa za Lishe ziingizwe katika kamati za kudumu za Halmashauri kwa ajili ya
kuzisimamia na kutolea maamuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu lishe.
4. Afisa lishe aandae mpango kazi wenye kutoa elimu, kutambulisha tatizo, kutoa njia ya kutatua na kufuatilia utekelezaji wake.
Kwa taarifa zaidi pakua nyaraka hizi:
Hotuba ya Mkuu wa Wilaya katika Kamati ya Lishe Wilaya ya Mpwapwa.pdf
Mada ya Lishe iliyowasilishwa na Afisa Lishe Wilaya ya Mpwapwa.pdf
Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.