(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Wilaya ya Mpwapwa leo imeadhimisha Wiki ya Maji Duniani ambapo kiwilaya imefanyika katika kijiji cha Mzase kata ya Berege. Katika Maadhimisho hayo Mgeni Rasmi ni Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Apolonia Temu akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri ambaye alikuwa katika majuku mengine na hivyo kushindwa kuhudhuria Sherehe hizi. Pia sherehe hizi zimehudhuriwa na wakuu wa idara mbalimbali toka katika Halmashuri ya Wilaya ya Mpwapwa wakiambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Khamlo Njovu Mkuu wa Idara ya Mendeleo ya Jamii akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Paul Sweya ambaye nae alikuwa katika majukumu mengine ya kitaifa. Aidha viongozi wa kata wakiwemo Waheshimiwa Madiwani wa kata ya Kingiti na Berege, pamoja na wananchi kwa ujumla wamejitokeza kwa wingi katika sherehe hizi.
Wananchi wa Kijiji cha Mzase wakisikiliza hotuba ya Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa katika Siku ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji
Kila mwaka Wiki ya Maji huadhimishwa kuanzia tarehe 16 Machi na kilele chake huwa ni Machi 22. Kiwilaya mwaka huu sherehe za kilele cha wiki ya maji zimefanyika katika kijiji cha Mzase kata ya Berege na ujumbe wa wiki ya maji kwa mwaka huu 2019 ni "Hakuna atayeachwa Kungeza kasi ya Upatikanaji wa Huduma ya maji Safi na Usafi wa Mazingira kwa Wote katika Dunia Inayobadilika Kitabia Nchi".
"Sherehe hizi zinafanyika katika Kijiji cha Mzase kwa kuwa ni miongoni mwa vijiji ambavyo kwa muda mrefu kulikuwa na upungufu wa huduma ya maji Safi na Salama", ameeleza Mhandisi wa Mji wa Wilaya ya Mpwapwa Eng. Christina Msengi.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa akiweka jiwe la msingi katika Ofisi ya Chombo Huru cha Watumiaji Maji kwenye Siku ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji katika Kijiji cha Mzase
Ndugu. Temu ameeleza kuwa; "Wilaya yetu inakadiriwa kuwa na watu wapatao 320,891 wanaoishi Vijijini, kati yao ni watu 161,000 ndio wanapata huduma ya maji safi na salama sawa na asilimia 51.17 kulingana na Sera ya Maji ya Taifa (NAWAPO) ya mwaka 2002. Wilaya inaendelea kutekeleza miradi 7 katika Vijiji vya Kidenge, Mzase, Iramba, Mima, Iyoma, Kibakwe na Bumila na inakarabati miradi 3 katika Vijiji vya Kingiti/Lukole, Chogola, na Seluka pamoja na kuchimba visima viwili virefu katika vijiji vya Mlunduzi na Bumila. Mpaka itakapokamilika itagharimu Tshs. 4,231,963,666.97 na jumla ya watu 42,057 watanufaika na huduma ya maji. Kukamilika kwa miradi hii kutaongeza kiwango cha utoaji wa huduma ya maji. Kukamilika kwa miradi hii kutaongeza kiwangoo cha utoaji wa Huduma ya Maji Vijijini kutoka asilimia 51.17 ya sasa hadi kufikia asilimia 64.3. maadhimisho haya yanakwenda sambamba na siku ya Maji Duniani (World Water Day) kwa kuzingatia Azimio la 47/193 la Umoja wa mataifa la mwaka 1992 linalotaka kila Nchi mwanachama kuadhimisha tarehe 22 Machi ya kila mwaka kama siku ya maji Duniani".
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa akiweka jiwe la msingi katika Ofisi ya Chombo Huru cha Watumiaji Maji kwenye Siku ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji katika Kijiji cha Mzase
Aidha Ndugu Temu amewaagiza viongozi wa kata, kijiji na wasimamizi wa Chombo Huru cha Watumiaji Maji (COWOSSO) baada ya mradi kukamilika kufanya yafuatayo:-
1. Kuhakikisha kuwa Chombo Huru cha Watumiaji Maji kinasimamia Uendeshaji na Matengenezo ya mradi wa maji bila kuingiliwa na Serikali ya kijiji. Ikumbukwe kuwa Chombo Huru cha Watumiaji Maji kinawajibika kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi kwa Uongozi na Jamii.
2. Kuhamasisha jamii kuhusu uchangiaji wa huduma za maji na uendeshaji wa mradi ili uwe endelevu.
3. Kuhamasisha jamii juu ya usafi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vilivyopo kwa kupanda miti, kutokulima au kuchunga mifugo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.
4.Uongozi wa Kijiji kwa kushirikiana na Chombo Huru cha Watumiaji Maji kusoma taarifa ya Mapato na matumizi kila baada ya miezi 3.
5. Kuhakikisha miradi ya maji inapatiwa vibali vya kutumia maji kutoka katika ofisi za bonde husika kwa mujibu wa Sheria ya Maji namba 11 ya mwaka 2009.
6. Kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyojengwa miundombinu ya maji yanatambuliwa na kuwa mali ya umma na kuwe na nyaraka zitakazothibisha.
7. Kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya ujenzi wa vyoo bora kulingana na mazingira yao na kuvitumia ipasavyo.
8. Kuhakikisha kuwa kila kaya inakuwa na choo bora na kukitumia na kuzingatia kanuni 5 za Afya.
Wananchi wa Kijiji cha Mzase wakisikiliza matangazo mbalimbali mara baada ya Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa kumaliaza kuhutubia katika Siku ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji
Wananchi wa Kijiji cha Mzase wamefurahi sana kwa upatikanaji wa maji katika kijiji hicho na wameeleza kuwa hapo awali kabla ya kupata mradi huu wa maji walikuwa wanaamka saa 10 alfajili kila siku kutafuta maji katika mabonde ya mito yaliyopo mbali na kijiji hicho. Pia Diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa Kijiji wote kwa ujumla wameishukuru sana Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutoa fedha ili wananchi hao wapate maji. Pia wananchi wa kijiji hicho wameaidi kuwa watatunza miundombinu ya maji na vyanzo vya maji kwa ujumla.
Mwisho Kaimu Katibu Tawala huyo amewakubusha wananchi wa Mpwapwa kwa ujumla kuwa kuwepo kwa maji bila ya kuyatunza vizuri ni kazi bure hivyotuhakikishe kuwa maji yanakuwa salama kwa afya bora.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.