Na: Shaibu J. Masasi; Afisa TEHAMA - Mpwapwa Dc.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Afisa Kilimo na Afisa Biashara, amefanya ukaguzi maalum wa kustukiza kukagua maduka ya wafanyabiashara wanaouza sukari bei ya juu tofauti na bei elekezi ya Serikali ya kuuza kilogram moja kwa Tsh. 2,900/=. Katika Ukaguzi huo umebaini kuwa wafanyabiashara wengi wa sukari wanauza sukari kilogram moja kati ya Tsh. 3,000/= hadi 3,200/= kinyume na maagizo na melekezo ya bei ya sukari yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Aidha ukaguzi huo umebaini baadhi ya wafanyabiashara kukiuka bei elekezi ya Serikali ya uuzaji wa sukari na hivyo Mkuu wa Wilaya ameagiza wote kukamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi na kuchukuliwa maelezo kwa ajili ya taratibu za kisheria ikiwemo na kuwapeleka mahakamani kwa ajili ya kuwafungulia mashtaka. Wafanyabiashara waliokamatwa ni pamoja na: Akyoo Sangito, Kitomali, Mwanamchiwa, Lekime, Mmasi, Rajabu Msenda, Joseph Temu, Liu, Getrude Mrema, mmiliki wa dula la El- Shadai lilopo Ilolo na Mmiliki wa duka la Uncle "D" katika eneo la Hazina.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri (kushoto) akikagua baadhi ya risiti zilizokatwa kwa wateja walionunua sukari katika moja ya duka lililopo Mpwapwa Mjini.
Vile vile katika ukaguzi huo Mhe. Shekimweri na timu yake amebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawana mashine ya EFD ya kutolea risiti kwa wateja, na walio na mashine hizo hawatumii, hivyo huuza bidhaa bila kutoa risiti za mashine ya EFD badala yake hutoa risiti ya karatasi toka katika vitabu walivyovitengeneza wenyewe. Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wafanyabiashaea hao kununua Mashine ya EFD kwa wale wasiokuwa nazo na walionazo wazitumie. Pia amemuugiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tawi la Mpwapwa kuhakikisha anafuatilia suala hili na kuumpa mrejesho.
Ingawa ukaguzi huu umefanywa kwa baadhi ya maduka makubwa yaliopo Mpwapwa Mjini tu, Mkuu wa Wilaya amesema kuwa "zoezi hili ni endelevu na linatarajiwa kufika katika maeneo yote ya Wilaya ya Mpwapwa kama vile Kibakwe, Pwaga, Kinusi, Mtera, Rudi na Chipogoro ili kuwakumbusha wafanyabiashara kufuata maagizo ya Serikali". Pamoja na kufanya ukaguzi huu Mkuu wa Wilaya ametoa elemu kwa baadhi ya wafanyabiashara kwa kusema wanapaswa kutii maagizo ya Serikali, sio mara zote itumike nguvu ya kuwalazimisha kufuata sheria na maagizo ya Serikali.
Hata hivyo katika ukaguzi huo umebaini baadhi ya wafanyabiashara wanafuata sheria na maelekezo ya Serikali ya kuuza shukari kwa bei elekezi, Mkuu wa Wilaya amewapongeza na kuwataka kutoa taarifa kwa wale wasiofuata maagizo ya Serikli ili washughulikiwe mara moja.
Mwisho Mkuu wa Wilaya ametumia ziara hii ya ukaguzi wa sukari kutoa elimu kwa wananchi kujilinda na ugonjwa hatari wa homa ya mapafu (COVID 19) unaosababishwa na virusi vya Corona. Pia ameongeza kuwa Wilaya yetu ipo salama mpaka leo ina watu wanaohisiwa kuwa na maambikizi ya virusi vya corona 21 ambao wapo karantini na wagonjwa 3 ambao wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.