(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amezindua mpango wa uandikishaji na utoaji wa Vyeti vya Kuzaliwa bure kwa watoto chini ya miaka mitano, hayo yamefanyika leo katika Ukumbi wa Kliniki ya Watoto iliyopo katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa. Katika uzinduzi huo wazazi wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa bure.
Katika hotuba yake Mkuu wa Wilaya amesema "Kwanza nianze kusema ni haki ya mtoto kutambuliwa lakini zaidi ya hapo akishatambuliwa lazima apate nyaraka ya uthibitisho ya kutambuliwa kwake ambayo ni cheti cha kuzaliwa. Kwa wasiojua cheti cha kuzaliwa ni nyaraka ambayo kisheria hutumika kuthibitisha taarifa muhimu sana kwa mmiliki wa cheti hicho na hutumika maeneo mbalimbali kupata huduma za kijamii. Cheti cha kuzaliwa kina matumizi mengi, hutumika katika kuandikisha watoto wanaoanza elimu ya msingi na wale wanaojiunga na elimu ya sekondari na sasa hivi huwezi kupata nafasi ya kujiunga elimu ya juu pamoja na kupata mikopo kwa ajili ya masomo hayo. Vile vile cheti cha kuzaliwa ni kiambatanisho cha msingi ili kupata nyaraka nyingine za utambulisho kama kadi ya kupiga kura, kitambulisho cha taifa, pasi ya kusafiria, leseni ya udereva kote huku utataikiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa ili kuthibitisha mahali na tarehe uliyozaliwa".
Wazazi wenye watoto chini ya miaka mitano wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa katika siku ya Uzinduzi wa Uandikishaji na Ugawaji wa Vyeti kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Ukumbi wa Kliniki ya Watoto Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Aidha Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa, pamoja na niliyoyataja hapo juu, cheti cha kuzaliwa pia ni muhimu ili kupata kazi serekalini na katika majeshi ya ulinzi na usalama nchini. Na katika zama hizi ambapo matibabu kwa wananchi wanatumia Mifuko ya Bima ya afya, cheti cha kuzaliwa hutumika kubainisha mahusiano kati ya wanafamilia. Umuhimu nilioutaja ni sehemu tu ya matumizi mengi ya cheti cha kuzaliwa hivyo ni muhimu kila mwananchi kuwa na cheti cha kuzaliwa bila kujali umri wake. Hata wazee wanahitaji cheti cha kuzaliwa sababu sasa hivi katika kumiliki ardhi serikali inahitaji kujua nani anayemiliki na hapo cheti cha kuzaliwa hutakiwa.
Usajili wa vizazi ni huduma muhimu sana kwa mwananchi mmoja mmoja lakini pia kwa Serikali ambayo hupata takwimu sahihi za idadi ya watu kwa ajili ya mipango ya maendeleona kuepuka matumizi ya takwimu za makisio. Hali hii inatokana na ukweli kwamba hatukuwa na mfumo madhubuti unaonakili matukio muhimu mara yanapotokea hivyo kuendelea kutegemea Takwimu za sensa ya Idadi ya watu na makazi ambazo ni makisio zinazofanyika kila baada ya miaka kumi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa akipata maelezo toka kwa wataalam jinsi ya kuandikisha na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano katika siku ya Uzinduzi wa Uandikishaji na Ugawaji wa Vyeti hivyo katika Ukumbi wa Kliniki ya Watoto Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Kama wote tulivyosikia katika hotuba ya mkurugenzi wa Halmashauri, ni wananchi asilimia 13.4 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Hizi ni takwimu za nchi lakini naamini ndio taswira ya hali ilivyo katika halmashauri yetu. Hii sio hali nzuri kabisa ukizingatia umuhimu mkubwa wa nyaraka hii kwa wananchi na nchi kwa ujumla. Kumekuwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha hali hii na serekali tayari imekwisha tafuta muarobaini na sasa nina uhakika baada ya muda mfupi ujao takwimu zetu zitakuwa bora sana na kila mwananchi atakuwa anatambuliwa katika mifumo ya serikali.
Mpango wa Usajili wa Watoto walio na Umri chini ya Miaka mitano katika Mpwapwa umezinduliwa leo. Huu ni mpango muhimu sana unaoleta suluhisho kwa changamoto zilizokuwa zinasababisha wananchi wengi kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa na kubwa ni ile ya umbali na sasa huduma zinanza kupatikana karibu kabisa na maeneo yetu ya makazi yaani katika vituo vya Tiba na Ofisi za watendaji kata. Naamini kabisa wananchi wote wanauwezo wa kufika katika moja ya vituo hivyo hakutakuwa na sababu ya kuwa na watoto wasio na vyeti vya kuzaliwa. Pamoja na umbali, vilevile vyeti hivi vinatolewa bila malipo yaani bure. Naomba ieleweke kwamba kutolewa kwa cheti hiki bure sio kwamba hakina thamani bali kina hadhi sawa na vyeti vingine na kwamba serikali na wadau wa maendeleo wanalipia gharama ili kila mtoto asajiliwe na kutambulika. Tunaishukuru sana serekali na wadau wote walioamua kubeba mzigo wa gharama kwa niaba ya mwananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa akikabidhi vyeti vya kuzaliwa kwa wazazi wenye watoto chini ya miaka mitano katika siku ya Uzinduzi wa Uandikishaji na Ugawaji wa Vyeti hivyo katika Ukumbi wa Kliniki ya Watoto Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Khamlo Njvu ameeleza kwamba halmashauri yetu ina jumla ya watoto wanaotakiwa kusajiliwa katika kipindi cha awali cha kampeni. Katika kikao cha utangulizi cha viongozi wa mkoa kuhusu mpango huu Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliweka lengo kuwa watoto wote mkoani kwake ni lazima wasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Kwa hiyo hapa katika halmashauri tunachukua lengo lile lile la kusajili watoto wote kwa asilimia 100. Nakuagiza Mkurugenzi na viongozi wengine wote kila mmoja katika nafasi yake akahakikishe kwamba lengo hili linafikiwa na nitatapotakiwa kupeleka ripoti niweze kutembea kifua mbele.
Mkuu wa Wilaya amewataka wanahusika na zoezi hili kuwa wadilifu, pia ameongeza kuwa nimepata taarifa kwamba kila kituo kina wasajili wasaidizi wasiopungua wawili ambao ndio wanatoa huduma za usajili. Naomba viongozi muwafikishie salamu kwamba wazingatie mafunzo waliyopewa na wasimame katika uadilifu kwa kuwasajili wale tu wanaostahili kwa mujibu wa sheria.
Pia huduma hii ni BURE na tuwakumbushe wasajili wasaidizi wasitumie mpango huu kama fursa ya kujipatia kipato na ninaeleza hili kwa sababu kuna mikoa baadhi ya wasajili ambao hawakuwa waaminifu walianza kuwatoza fedha wananchi kinyume na maelekezo waliyopewa. Kama Mkuu wa Wilaya natoa maelekezo kwamba yoyote atakayekiuka misingi ya utendaji ya mpango huu kwa makusudi hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria. Kila kituo kimepewa simu kwa ajili ya kutuma taarifa. Wasajili katika vituo wahahakikishe wanazitunza na kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa kwani yapo maeneo ambayo wasajili walizigeuza simu hizo kuwa za matumizi binafsi.
Mpango huu umeletwa na RITA kwa ajili wa Wananchi wa Mpwapwa, hivyo Mkuu wa Wilaya amewasihi wananchi kuchangamkia fursa hii kuwasajili watoto na kuhakikisha kama kuna jirani unafahamu ana mtoto wa umri chini ya miaka mitano unamuuliza kama amekwisha kumsajili. Kila mmoja akawe balozi katika eneo lake na wape uhakika kwamba vyeti vinavyotolewa ni halali na watoto watavitumia muda wote wa maosha yao na sio kwamba kwa sababu kinatolewa kwa watoto wa umri huo basi wakifika miaka mitano kinakuwa hakitumiki tena. Sio kweli hiki ni cheti cha kudumu.
Kwa niaba ya wananchi, Napenda kuishuru serikali kwa kuleta mpango huu katika eneo letu. Pia naipongeza RITA kwa juhudi inazofanya katika kuleta mabadiliko chanya katika masuala ya usajili. Miaka ya nyuma nakumbuka ilikuwa kupata cheti cha kuzaliwa ilichukua mpaka miezi sita lakini sasa tumeona jinsi maboesho haya yanavyoleta mapinduzi makubwa. Vilevile, nawashukuru wadau wa Maendeleo ambao wameshirikiana na serikali kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huu unaendelea kutekelezwa. Shirika la Watoto la Umoja wa MataifaSerikali ya Kanada,Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO .
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amesema, Tunathamini sana kazi mnayoifanya katika nchi yetu. Binafsi nategemea kuanza ziara ya kukagua utekelezaji wa mpango huu katika maeneo mbalimbali ya wilaya yangu ili kuhakikisha tunafikia lengo letu kama wilaya.
Mwisho, nawashukuru wananchi wote mliohudhuria uzinduzi huu. Naamini mmepata ujumbe na maelezo ya kina kuhusu Mpango huu na naomba mkawe mabalozi wazuri katika maeneo mnayoishi.
Kwa taarifa zaidi Pakua nyaraka hii:
HOTUBA YA MKUU WA WILAYA KATIKA UFUNGUZI WA VYETI VYA KUZALIWA VYA WATOTO CHINI YA MIAKA MITANO.pdf
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.