(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa wamejitokeza kwa wingi katika Siku ya Usafi Duniani kwa kufanya usafi katika maeneo yote ya wilaya pamoja na maeneo ya Soko Kuu la Mpwapwa Mjini na Kituo cha Mabasi. Makundi yaliyojitokeza katika kufanya usafi katika siku hii maalum ni pamoja na Jeshi la Magereza, Jeshi la Kutenga Taifa (JKT), Jeshi la Polisi, Jeshi la Akiba (Mgambo), Vijana wa Skauti, Wafanyabiashara, Wakuu wa Idara wakiongozwa na Ndug. Khamlo Njovu; Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii pia akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Waheshimiwa madiwani wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime, Watendaji wa Kata na Vijiji, na wananchi kwa ujumla.
Katika kuadhimisha siku hiyo, makundi yote yaliyojitokeza wamefanya usafi kwa pamoja na kufanikiwa kukusanya taka nyingi kutoka kila kona ya Wilaya yatapa kama ujazo wa gari aina ya tipa tano na kuzipeleka eneo la kuzitupa na kuteketeza taka.
Aidha katika kufanikisha siku hii maalam na kufanya usafi madhubuti shirika la NIPEFAGIO limetoa vitendea kazi kwa ajili ya kufanyia usafi ikiwemo mifuko ya kuhifadhia na kubebea taka.
Wananchi wa Mpwapwa wakiwa katika harakati za kufanya usafi katika eneo la Soko Kuu Mpwapwa Mjini.
Baada ya zoezi la kufanya Usafi kuisha, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ambaye pia ni Afisa Tarafa wa tarafa ya Mpwapwa Ndug. Obert Mwalyego alipata fursa ya kuongea na wananchi kwa kuwashukuru kwa kuhudhuria na kufanya usafi, na kuagiza yafuatayo:-
1. Kila jumamosi wananchi wote wa Wilaya ya Mpwapwa wanatakiwa kufanya usafi katika maeneo yao ya kazi na nyumbani.
2. Kila mwananchi katika nyumba yake na mahali pa kazi/biashara ahakikishe anakuwa na chombo cha kitunzia taka.
3. Mwananchi asiyefanya usafi katika eneo lake kwa kila siku ya jumamosi atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo na kutozwa faini.
Pia Ndug. Mwalyego amesisitiza kuwa siku ya jumamosi ya kila wiki ambayo sio jumamosi ya mwisho wa mwezi wananchi wafungue biashara zao mapema ila wawe wameshafanya usafi katika maeneo yao. "Lakini siku ya jumamosi ya mwisho wa mwezi itakuwa kama kawaida biashara zitafunguliwa kuanzia saa nne asubuhi baada ya usafi". alisisitiza.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.