Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amefanya ziara katika Bonde la Lumuma kukagua fursa mbalimbali zinazopatika katika Bonde hili ambalo ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu. Mkuu wa Wilaya ameambatana na wadau wa Kilimo toka taasisi na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi kwa ajili ya kutembelea Bonde la Lumuma lililopo Kata ya Lumuma Wilayani Mpwapwa ili kujionea fursa za uwekezaji hasa katika shughuli za kilimo na mazao ya kilimo.
Wadau wa kilimo ambao wameambatana na msafara huu wa Mkuu wa Wilaya ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Mwakilishi wa TCIA Wilaya, Wataalam toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wataalam toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Meneja wa Benki ya NMB, Wafadhiri wa Miradi toka LIC, SIDO, Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Mwakillishi wa Baraza la Biashara Wilaya, Mwakillishi wa Baraza la Biashara Mkoa, Maafisa Biashara na Kilimo pamoja na wataalam toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa (wa tatu kulia) akiwa na wadau wa kilimo kuwatangazia wananchi wa Lumuma fursa mbalimbali zinazotokana na bonde hilo
Katika Bonde la Lumuma Mradi wa LIC umefadhiri ujenzi wa mfereji wa umwagiliaji katika mashamba ya vitunguu, mahindi, maharage na mazao mengine yanayozalishwa katika Bonde hili wenye urefu wa Meta 5,000 na una thamani ya Shilingi Milioni mia mbili arobaini na tano (Tsh. 245,000,000.00). Mfereji huo upo katika hatua za ujenzi ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba 2018. Mfereji huo unatarajiwa kuhudumia vijiji viwili vya Mafene na Kitati vyote vikiwa katika bonde la Lumuma. Ujenzi wa Mfereji huu utaboresha tija ya uzalishaji na hivyo kupanua wingi wa upatikanaji wa bidhaa za kilimo zinazozalishwa katika bonde hili. Vile vile itachochea shughuli za biashara na kuvutia wawekeazji toka nje na ndani ya Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (kwanza kulia) akipata maelezo ya maradi wa ujenzi wa mfereji wa umwajiliaji toka kwa Afisa Kilimo - Umwagiliaji wa Wilaya
Katika ujenzi wa mfereji huu, wananchi hawakuwa na uelewa wa kutosha japo walielimishwa juu ya ushirki wao katika kujitolea nguvu kazi, hivyo imesababisha mradi kutojengwa kwa kasi na kukamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa, kufuatia hali hii Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ametoa agizo kila mwananchi wa Lumama kama mnufaika wa maradi huu wa mfereji wa umwagiliaji ajitolee kukusanya mawe na mchanga na ifikapo mwezi Disemba 2018 mradi uwe umekamilika.
Aidha kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kupeleka lori Lumuma kwa ajili ya kusomba mchanga na kokoto ili kufanikisha ukamilishaji wa mfereji kwa wakati uliopangwa.
Mratibu wa LIC Bw. Ibrahimu amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuona kasi ya ujenzi wa Mfereji kusuasua na hivyo kuingilia kati ili kufanikisha ujenzi huo umkamilike kwa wakati. Pia amehaidi kuwa wafadhiri wako tayari kutoa fedha kwa wakati kadri kazi inapofikia hatua flani na hakuna ucheleweshwaji wa fedha katika mradi huu.
Bonde la Lumuma likiwa limepandwa mazao ya maharage, Mahindi, mbogamboga, migomba, vitunguu na mzao mengine.
Vitunguu vikiwa vimewekwa katika magunia kwa ajili ya kusafirishwa kwenda sokoni, (wa kwanza kushoto) Mkuuwa Wilaya ya Mpwapwa
Wadau mbalimbali walioambatana na Mkuu wa Wilaya wamesema wako tayari kuwawezesha wakulima wa Lumuma katika mambo muhimu kama vile Wadau toka SIDO wamesema wako tayari kutoa Mikopo ya Mashine mbalimbali na zana za kilimo kwa bei nafuu, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wamesema wako tayari kutoa mikopo ya fedha, pembejeo na zana za kilimo yenye riba nafuu ambapo wakulima watarejesha marejesho baada ya mavuno, wadau toka Benki ya NMB wamesema wako tayari kwa kuwafungulia akaunti wakulima zenye bei nafuu maarufu kama Chapuchapu akaunti na watawafuata wakulima Lumuma na sio wakulima wasafiri kwenda mjini benki ilipo, wadau toka mradi LIC wamesema wako tayari kuendelea kuwawezesha wakulima wa Lumuma katika kilimo cha umwagiliaji na kuleta miradi mingine mingi ya kadri inavyohitajika ili kukuza tija katika kilimo cha wakulima wa Lumuma na wadau toka Baraza la Biashara wamesema wako tayari kuwawezesha wakulima wa Lumuma kuunda vikundi au vyama vya wakulima na kuwatafutia masoko kwa ajili ya bidhaa zao.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amewapongeza wadau wa Kilimo kwa kutangaza fursa hizo na amewataka wakulima wa Lumuma kuchangamkia fursa hizo zilizotangazwa. Pia Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa mkakati wa baadae ni kuanzisha Mnada maalum kwa ajili ya mazao ya vitunguu Lumuma ila wakulima wasiuze bidhaa zao kwa bei ya hasara kwa walanguzi.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.