Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo amezindua mafunzo ya michezo kwa walimu wote wa michezo wa shule za msingi na sekondari zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Mafunzo haya yamezinduliwa katika kituo cha Shule ya sekondari ya Mpwapwa, ambapo katika mafunzo haya kumeandaliwa vituo viliwili vilivyounganishwa tarafa na hivyo kuwa na kituo cha tarafa ya Kibakwe na Mpwapwa. Michezo inayofundishwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa mkono, mazoezi ya viungo, kuongoza michezo (coaching) na tiba kwa wanamichezo.
Walimu wanaoshiriki katika mafunzo ni kama ifuatavyo:- tarafa ya Mpwapwa wanaoshiriki ni walimu 35 kati ya walimu waliotarajiwa kushiriki 58 sawa na shule 18 kati ya shule 35 zilizotarajiwa kushiriki, tarafa ya Mima washiriki ni walimu 12 kati 17 sawa na shule 9 kati 13 zilizotarajiwa kushiriki, tarafa ya Kibakwe walimu washiriki ni 22 kati ya walimu 57 waliotarajiwa kushiriki sawa na shule 14 kati shule 37 zilizotarajiwa kushiriki, tarafa ya Rudi walimu wanaoshiriki ni 26 kati ya walimu 44 waliotarajiwa kushiriki sawa na shule 18 kati ya 32 zilizotzrajiwa kushiriki. Kwa ujumla idadi ya walimu wote Wilaya nzima wanaoshiriki katika mafunzo haya ni 53%, na kwa upande wa shule zinazohudhuria mafunzo kwa wilaya nzima na sawa 50% ya shule zote. Kwa upande wa shule za sekondari ni shule 3 tu zinahudhuria kati ya shule 26 za sekondari zilizopo katika wilaya ya Mpwapwa.
Mafunzo haya yanafundishwa na wataalam wa michezo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Mkoa wa Mwanza. Wataala hao wa michezo wanatarajiwa kufundisha michezo ya aina mbalimbali kama vile mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa mkono, mazoezi ya viungo, kuongoza michezo (coaching), riadha na tiba kwa wanamichezo.
Aidha, mafunzo haya yamehudhuria na wadau wa michezo toka Mkoani Dodoma, Mwanza na wengine toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Mafunzo haya yatafanyika kwa siku kumi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (aliyesimama) atoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo wa michezo yanayotolewa na Mkufunzi toka chuo cha Michezo cha Malya - Mwanza kwa walimu wa michezo wote wa shule za msingi na sekondari Wilayani Mpwapwa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Mpwapwa .
Mkuu wa Wilaya Mhe. Shekimweri katika hotuba yake amesisitiza kuwa, vijana kujihusisha na michezo ili kuwa wakakamavu na kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya. Pia amesikitishwa sana na kupata washiriki wachache kwa upande wa shule za sekondari, na amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kupata maelezo kwa nini upande wa sekondari washiriki ni wachache.
Pia amesema katika hawa walimu waliohudhuria wapatikane walimu waliopata mafunzo vizuri ili wakawafundishwe walimu wasiohudhuria katika mafunzo haya. Vile vile ameagiza kuwa kila mshiriki aandae mpango kazi wa namna ya kuwafundisha wengine katika shule yake ili kuwa walimu wote wenye taaluma ya michezo, hii ni kwa sababu tutakuwa michezo ya UMISHUMTA na UMISETA kwa mwaka 2019 hivyo tujiandae vizuri kupitia mafunzo haya.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wapili kulia) akiwa katika mazoezi ya pamoja na walimu wa michezo wa shule za msingi na sekondari za Wilayani Mpwapwa mara baada ya kufungua mafunzo hayo katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa
Pia Mhe. Shekimweri amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Khamlo Njovu ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mpwapwa kuwa kila shule iboreshe viwanja vya michezo kwa kuweka vipimo stahiki kulingana na vipimo vya kimataifa na kuwawezesha kupata vifaa vya michezo vya kisasa. "Sisi kama wilaya tumeanza maandalizi ya kuboresha kiwanja chetu cha Michezo cha Mgambo kwa kuweka sehemu ya gym, ofisi ya michezo, restaurant na michezo mbalimbali pamoja na vifaa vya michezo vya kisasa ili kila mtu aweze kufanya mazoezi" ameeleza Mhe. Shekimweri.
Walimu wa michezo wa shule za msingi na sekondari za Wilayani Mpwapwa walisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa
Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.