(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa leo amefanya ziara katika kata ya Lupeta na Mpwapwa Mjini kwa ajili ya kukagua shughuli za utayarishwaji wa mashamba katika msimu huu wa kilimo, na amekutana na wakulima wa maeneo hayo. Katika hotuba yake kwa wananchi wa maeneo hayo Mkuu wa Wilaya amewahimiza na kuwakumbusha wakulima kuwa msimu wa kilimo unakaribia hivyo kila mwananchi aanze kuandaa mashamba. Pia amesisitiza kuwa kila kijana mwenye uwezo wa kufanyakazi awe na shamba la mzao ya chakula na mazao ya biashara hasa zao la korosho.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabir Shekimweri akiuchunguza mche wa mkorosho ukiwa umeanza kutoa maua, hii ni baadhi ya miche ya kisasa iliyopandwa mwaka 2017 katika shamba la mkulima mmoja kata ya Lupeta
Aidha Mkuu wa Wilaya amewaagiza maafisa Kilimo wa Kata kuhakikisha wanawasaidia wakulima kwa kuwapa maelekezo ya kitaalamu Katika upandaji na usimamizi wa zao la korosho ili liwe na tija kwa wakulima hao.
Mhe. Shekimweri ametoa maagizo hayo Jana Katika ziara ya ukaguzi wa mashamba ya korosho na uandaji wa viriba vya mbegu za korosho unaoandaliwa na kikundi cha akina Mama Wilunze kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019. Pia amesema Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 aliiagiza kila kijiji kuwa na shamba darasa la korosho jambo alilosema bado halijatekelezwa kwa vijiji vingi vya Mpwapwa na awataka mwaka huu kutekeleza.
Aidha Shekimweri amewaomba madiwani na viongozi wote wa kuteuliwa na kuchaguliwa kuihimiza jamii juu ya mabadiliko ya Mpwapwa mpya inayolenga katika mabadiliko ya kiuchumi kwa kuwa na zao mkakati la Wilaya linalo lenga kuinua uchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii ikiwemo Elimu, afya na huduma za maji.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabir Shekimweri (katikati) akiwa na Afisa Kilimo wilaya Bi. Maria Leshalu (kulia) wakikagua mashamba yaliyotayarishwa na wakulima katika msimu huu wa kilimo kata ya Lupeta
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo Bi. Maria Leshalu amesema kama zao la korosho likatikiwa mkazo na kufuatiliwa kwa kanuni za kilimo, basi jamii ya Mpwapwa ndani ya miaka mitano ijayo itaimarika kiuchumi na kimazingira. Amesema wananchi lazima wafuate maelekezo ya wataalamu ili kuweza kupata tija katika zao hili.Pia Afisa Kilimo huyo amewataka wananchi kuweza kuzingatia taarifa za hali ya hewa ili kuweza kuandaa mashamba yao kwa msimu wa kilimo kwa mwaka 2018/2019.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabir Shekimweri (kushoto) akikagua kitaru cha miche ya mikorosho ikiwa katika viriba kama maandalizi ya wakulima katika msimu huu wa kilimo eneo la Mji Mpya kata ya Mpwapwa Mjini
Mmoja wa wananchi ambao ni wakulima wa korosho amesema upatikaji wa dawa za kupiga katika zao hilo kunatishia uzalishaji kupungua na baadhi ya miche kunyauka. Kutokana na changamoto hiyo, Afisa Kilimo wa Wilaya ameahidi kuishughulikia mara moja hasa katika upatikanaji wa dawa za kuua wadudu na kutibu magonjwa ya korosho.
Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.