(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Viongozi waliochaguliwa katika Uchuguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa leo wameapishwa rasmi ili kuanza kazi mara moja ya kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa na watanzania kwa Ujumla.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kulikuwa na nafasi za wenyeviti wa vijiji 113, wenyeviti wa vitongoji 591, wajumbe wa viti maalam wanawake 904, na wajumbe wa halmashauri ya Kijijini Mchanganyiko 1217. Hivyo jumla ya wagombea katika nafasi zote kuwa 2825. Katika nafasi zote nne vyama vilivyoshiriki katika Uchaguzi huo vilikuwa ni viwili tu navyo ni: Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Viongozi na Wasimamizi wa uchaguzi wakiwa mbele kwa kutoa maelekezo kabla ya kuwaapisha viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Viongozi hao ni Ndugu Khamlo Njovu Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya (wa pili kushoto), Ndugu. Nelson Nyange Afisa Mtendaji (kushoto) wa Kata ya Vinghawe, Mhe. Debora M. Mnyabahi Hakimu Mkazi (wapili kulia) na Ndugu. Maria Leshalu Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Wilaya (kulia).
Aidha kabla ya kuwaapisha viongozi hao waliochaguliwa Mhe. Mnyabahi Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mpwapwa amesema "ninawaapisha leo ili mkatende haki na muwe waadilifu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla, kiongozi yoyote atakayeenda kinyume na kiapo hiki atachukuliwa hatua kali za kisheri." Pia ameongeza kwa kuuliza swali kuwa Je, kuna kiongozi yeyote hataki kuapa? viongozi wote wamejibu wakotayari kuapa ili kuwatumikia wananchi wa Mpwapwa na taifa kwa ujumla.
Mhe. Debora M. Mnyabahi Hakimu Mkazi (kushoto) akiwaapisha wajumbe wa viti maalam wanawake walioshinda Uchaguzi wa Mwaka 2019, hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Mwanakianga
Katika matokeo ya Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 uliofanyika Mpwapwa kulikuwa na matokeo ya aina mbili; moja ni Matokeo ya Uchaguzi kwa Wagombea waliopita bila kupingwa na pili ni matokeo ya Uchaguzi baada ya wagombea kupigiwa kura. Kati ya kata 33 za Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, ni kata mbili tu ndio wagombea wake walipigiwa kura katika Kata ya Kimagai kijiji cha Kimagai na Kata ya Pwaga kijiji cha Maswala. Hivyo kata 31 na vijiji 111 wagombea wake walipita bila kupingwa.
Akipongeza jinsi mchakato wa uchaguzi ulivyoendeshwa kwa amani na haki Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Khamlo Njovu amesema "nawashukuru na kuwapongeza wagombea wote kwa kushiriki uchaguzi kwa amani bili vurugu, pia nawasihi baada ya kuapishwa mkafanyekazi kwa bidii ili kuleta maendeleo katika Wilaya yetu bila kubaguana maana maendeleo hayana chama, dini wala kabila". Ndugu Njovu ameongeza kuwa "shirikiananeni na washindani wenu mliogombea pamoja na kisha wakashindwa na viongozi waliomaliza muda wao ili kuleta maendeleo na kukuza dhana ya ushirikishaji jamii".
Viongozi walioshinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, wakijaza fomu za viapo muda mfupi baada ya kuapishwa na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mpwapwa katika Vifanja vya Shule ya Sekondari Mwanakianga.
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi huo nafasi zote zilichukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), nafasi zilizopita bila kupingwa ni wenyeviti wa vijiji 113, wenyeviti wa vitoongoji 588, wajumbe wa viti maalam wanawake 904 na wajumbe mchanganyiko 1210. Pia kwa nafasi zilizopigiwa kura za kata ya Kimagai na Pwaga ambazo pia chama cha CCM kimeshinda.
Mmoja wa viongozi walioapishwa ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Kota kupitia chama cha CCM Ndugu. Omari Kubenea amesema " nawashukuru wananchi wa kitongoji cha Kota kwa kunichagua na anaahidi kuwa nitateleza jukumu hili kwa kufuata sheria za nchi hii na kanuni zilizowekwa. Pia nitakumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John P. Magufuli kwa kufanyakazi kwa bidii ili kulendeleza juhudi zake na kuleta maendeleo katika Nchi hii".
Mwisho, hakimu mkazi amewasihi viongozi walioapishwa kuwa wasisite kuuliza katika kufanya maamuzi yenye utata na kufuata miongozo na sheria zilizowekwa, hivyo waendelee kujifunza ili wasijikute wanaangukia katika mikono ya dola.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.