TAYOA (Tanzania Youth Alliance) ni shirika lisilo la kiserikali lilianzishwa Novemba 1997 na kupata namba ya usajili 1497 likiwa makao yake makuu Masasani Beach kitalu namba 889/890 Dar es Salaam. Shirika hili lilianzishwa sio kwa lengo la kupata faida ila ni kwa lengo la kuwasaidia vijana waishio mjini na vijijini kupata taarifa mbalimbali kupitia Teknoloji ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). (Chanzo: Tovuti ya TAYOA ambayo ni www.tayoa.org).
Mwezeshaji toka TAYOA akitoa mafunzo kwa wadau waliohudhuria mafunzo hayo katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa tarehe 19 Julai, 2018. (Picha. Na. Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mafunzo haya ya TAYOA yamefanyika leo katika ukumbi wa wilaya ya Mpwapwa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wazee maarufu, baadhi ya waheshimiwa madiwani, maafisha elimu, wafanyakazi wa idara ya maendeleo ya jamii, viongozi wa chama cha walemavu na watendaji wa kata.Lengo la kuu la mafunzo haya ni kutoa elimu kwa wadau hao ili waweze kuwaelimisha wasichana walioko shuleni kuendelea kupata elimu na walio nje ya mfumo wa elimu kupata mbinu mbadala za kujikimu kimaisha wakiwa salama dhidi VVU na UKIMWI.
Aidha mwezeshaji amefafanua mambo ya msingi yanayosimamiwa na shirika la TAYOA ni :-
1.Kutekeleza programu za VVU/UKIMWI katika mabadiliko ya tabia (Behavioral Change).
2.Kutekeleza Programu za VVU/UKIMWI za Kitabibu (Bio-Medical).HTC
3.Kutekeleza Programu za VVU/UKIMWI kwa masuala Mtambuka (Structural).
4.Kutekeleza Programu za VVU/UKIMWI kwa misingi ya Jinsia na Haki za Binadamu (Human rights and Gender) GBV
Mhe. George Fuime Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa (aliyesimama mbele) akichangia mada katika mafunzo yanayotolewa na TAYOA 19 Julai 2018. (Picha. Na. Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine imepata usaidizi wa Fedha kutoka Mfuko wa Dunia (Global Fund-GF) kwa ajili ya kuendeleza miradi ya mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) na athari za UKIMWI nchini kwa kipindi cha Januari 2018-Desemba 2020. Kwa kipindi hicho mradi umelenga miradi midogo kama ifuatayo:-1. Mradi wa GF kwa Tanzania Bara umelenga vipaumbele (thematic areas) 11 kuhusu kinga dhidi ya VVU na athari za UKIMWI.
2. Mradi wa GF utatekelezwa na Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchi nzima kwa kipindi cha miaka mitatu (Januari 2018-Desemba 2020).
3. Mradi wa Kinga dhidi ya VVU na athari za UKIMWI kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana ndani na nje ya shule (Adolescent Girls and Young Women-AGYW in schools and out of schools)
4. Mradi wa VVU na UKIMWI.
Mradi huu utatekelezwa katika mikoa 3 ya majaribio kwa kipindi cha Januari 2018-Desemba 2020 kwa Tanzania Bara; katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida. Walengwa wakuu wa Mradi huu ni Wasichana Balehe na Wanawake Vijana wenye umri kati ya miaka 10-24 walio ndani na nje ya shule. Watekelezaji wa Mradi wa AGYW ni Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), NACP, AMREF, TASAF, TAYOA na WAMJW. Pia TACAIDS itaratibu utekelezaji wa mradi wa AGYW.
Mhe. George Fuime Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa (wakati mbele) akiwa na wadau wengine wa mafunzo hayo mara baada ya kumaliza mafunzo ya siku 2 ya TAYOA 19 Julai 2018. (Picha. Na. Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mwezeshaji ameeleza kuwa mradi umewalenda sana wanawake balehe wenye umri kuanzia 10 - 25 n kutokana na Sensa ya Watu na Makazi (2012) kwa Tanzania inaonesha kundi la vijana chini ya miaka 24 ni takribani asilimia 63 ya idadi ya Watanzania wote.
Maambukizi mapya ya VVU kwa jamii yote yameendelea kushuka ikijumuishwa na kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 kwa asilimia 18 kwa kipindi cha miaka 3 iliyopita.
Hata hivyo, uwiano wa maambukizi mapya ya VVU kwa vijana wenye umri kati 15-24 yameendelea kuwa juu kwa asilimia 31 ukilinganisha na maambukizi yote (2015 Spectrum estimates).
Kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kwa vijana balehe na vijana (10–24) ni 40%. Kati ya hayo maambukizi, 80% yanatoka kwa kundi la Wasichana Balehe na Wanawake Vijana (THIS, 2016/17).
Hatari ya Maambukizi ya VVU kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana yanachangiwa na sababu kuu 3 ambazo ni; sababu za kitabia (behavioral), za kibaiolojia (biological) na mtambuka (structural).
Umaskini wa kipato katika kaya unawaweka Wasichana Balehe na Wanawake Vijana katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kwa kushiriki ngono zisizo salama ili kupata kipato.
Kundi hili linajumuisha wasichana kutoka katika kaya maskini ambao wamekatisha masomo kutokana na umaskini.
Wasichana waliokatisha masomo hawapati mbinu mbadala za kujikimu kimaisha zikiwemo stadi za maisha na ujasiriamali; hivyo kuwa kwenye hatari ya kushiriki biashara ya ngono ambayo ni kichocheo kikubwa cha maambukizi ya VVU.
Kutokana na kufanya ngono zisizo salama, kundi hili lipo kwenye hatari ya kupata mimba za utotoni, kuolewa katika umri mdogo na kufanyiwa vitendo vingine vya ukatili vinavyochangia uwezekano wa kupata maambukizi ya VVU.
Kutokana na changamoto hizo, Serikali kupitia usaidizi wa GF, imeamua kuanzisha na kuendeleza programu za VVU na UKIMWI kwa kundi la Wasichana Balehe na Wanawake Vijana kupitia afua zifuatazo:-
a.Kubadili tabia,
b.Programu za upimaji wa VVU na matibabu ya UKIMWI,
c.Programu za Afya ya Uzazi,
d.Programu za kuondoa umaskini wa kipato na
e.Programu nyingine mtambuka.
Katika kupunguza umaskini wa kipato, mradi huu utalenga kaya maskini zaidi kama zilivyoanishwa na zitakavyokuwa zikiainishwa na programu ya kunusuru kaya maskini inayoratibiwa na TASAF, kwa kutumia mfumo wa utoaji wa ruzuku kwa kaya maskini zaidi (cash tranfer).
Programu ya kunusuru kaya maskini inalenga watoto waliopo shuleni na wale walio nje ya mfumo wa shule ili kutoa huduma zinazoendana na mahitaji kwa kuzingatia umri wao kupitia kaya maskini.
Kwa ujumla, wasichana Rika na wasichana Balehe (Adolescent Girls and Young Women) wapo kwenye hatari kubwa kuendelea kupata maambukizi ya VVU, lakini upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI umeendelea kuwa duni.
Pia, Elimu ya Afya ya Uzazi kwa kundi hili haijapewa kipaumbele ikilinganishwa na watu wazima (TDHS 2015-16).
Kwa taarifa zaidi pakua nyaraka hizi:
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.