(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Wanawake wa Wilaya ya Mpwapwa leo wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo siku hiyo huadhimishwa kila Mwaka tarehe 8 Machi, kiwilaya siku hiyo imeadhimishwa kwa maandamano kuanzia viwanja vya shule ya Msingi Chazungwa hadi katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa. Kauli Mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Wilaya ya Mpwapwa ni "Badili Fikra Kufikia Usawa wa Maendeleo Endelevu".
Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Wanawake wa Wilaya ya Mpwapwa wameweza kupata fursa ya kuonyesha bidhaa wanazozitengeneza wenyewe pamoja na shughuli mbalimbali za ujasiliamali. Pamoja na kuadhimisha siku hiyo, Wanawake wa Mpwapwa wamewatembelea wanawake wanzao 10 waliofungwa katika gereza la Mpwapwa na kuwapatia mahitaji muhimu zikiwemo taulo za kike.
Wanawamke wakiwa katika Ukumbi wa Chuo cha Walimu cha Mpwapwa wakionyesha bidhaa zao walizozitengeneza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
Katika risala yao wanawake wa Mpwapwa wamemweleza Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya mambo mbalimbali waliyoyafanya ikiwemo wameanzisha vikundi vingi na wanaomba vikundi hivyo visajiliwe na kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali.
Aidha chimbuko la siku hii ni wanawake wa Marekani waliokuwa wanafanyakazi katika sekta ya viwanda waliokuwa wanapinga unyanyasaji wa kijinsia na mazingira duni katika kazi zao mwanzoni kwa mwaka 1900, na ilipofika Mwaka 1945 baada ya kuazishwa Umoja wa Mataifa uliridhia kuwa kila tarehe 8 Machi ya kila mwaka iwe ni siku ya wanawake Duniani. Umoja wa Mataifa uliridhia kwamba masuala ya wanawake yanahitaji msukumo wa kipekee na ndio maana ikawepo siku maalum ya kujadili masuala ya wanawake kama hivi leo. Siku hii imekuwa ni siku ya kuwakutanisha wanawake wote na sio wafanyakazi wanawake tu kama ilivyokuwa hapo awali huko Marekani.
Wanawake wa Mpwapwa wameanzisha Jikwaa la Wanawake ambalo limeanzisha mfuko na akaunti katika benki ya NMB kupitia michango yao na wadau wengine, mfuko huo umechangiwa na kuungwa mkono na wadau/taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za Benki, Chuo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa, Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mahakama, Polisi, CDF, Chuo cha Mifugo na wadau wengine walinaounga mkono.
Imeelzwa kuwa Wanawake wa Mpwapwa wanachangamoto za Kuongezeka kwa ukatili juu ya wanawake, kuongezeka kwa mimba za utotoni, ukosefu wa elimu juu ya afya ya mama na mtoto, Pia jukwaa la wanawake linaunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuleta maendeleo ya viwanda, kupinga matumizi ya madawa ya kulevya, mazoezi ya kila jumamosi ya pili ya kila mwezi na usafi wa mazingira wa kila mwisho wa mwezi.
Mkuu wa Wilaya akikagua na kupatiwa maelezo ya bidhaa zinazozalishwa na Wanawamke wa Mpwapwa katika Ukumbi wa Chuo cha Walimu Mpwapwa wakionyesha bidhaa wanazotengeneza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amepongeza jitihada hizi za wanawake kuwatembelea wenzao waliopo magereza na hapa anasema "Nawapongeza sana kwa kuwatembelea wanawake 10 kule gerezani, kwa kweli wanawake wale wanachangamoto nyingi. Mimi huwa nafanya ziara na kuongea na wafungwa ila kutokana na changamoto za wanawake wa kule gerezani wakati mwingine huwa namwambia Katibu Tawala wa Wilaya abaki kuongea na wanawake wenzie ili kufahamu changamto zao na kuzipatia ufumbuzi."
Mkuu wa Wilaya amewaasa wanawake kutumia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha zenye riba nufaa hususani benki, na kuachana na kukopa kwenye taasisi zisizotambulika kisheria. Pia amewataka kuzingatia ushauri wa namna ya kuingia mikataba kama alivyoelekeza Mhe. Hakimu wa Wilaya ya Mpwapwa ili kuweza kukopa katika taasisi sahihi na yenye masharti nafuu.
Mhe. Shekimweri, Mkuu wa Wilaya amesisitiza kuwa mwaka huu 2019 kutakuwa na Uchguzi wa Serikali za mitaa na mwaka 2020 ni Uchaguzi Mkuu, "mnatakiwa kuonyesha nia ya kugombea ili kufika 50% kwa 50%, na msishawishike kwa rushwa za ngono ili kuchaguliwa au kuaidiwa nafasi, wanawake pambaneni sifa mnazo; wanawake ni waaminifu, watunza familia, mnaushawishi na lugha ya mvuto katika kuzungumza hivyo mnaweza gombeeni" amesema Mkuu wa Wilaya.
Wanawamke wa Mpwapwa wakiwa katika Ukumbi wa Chuo cha Walimu Mpwapwa wakiwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
Pia Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa kuna program zinazendelea katika Wilaya yetu ikiwemo, Jiongeze Tuwavushe Salama, hii ni kampeni ya kuwaokoa wamama wajawazito na watoto wachanga, kila mmoja awajibike ili kutimiza mama mjamzito anajifungua salama, uwajibikaji huo uanze tangu katika Lishe kuwa anapata chakula bora, kwenye vyombo vya usafiri ukiona mama mjamzito amesimama mpishe ili akae, ukiwa na usafiri wako ukimuona mama mjamzito anatembea au amepata shida basi saidia kumpeleka hospitali, pia wakati wa kwenda kliniki baba na mama mjamzito waongozane kwenda kliniki ili kutapa huduma na ushauri wa kitaalam katika masuala ya afya ya mama na mtoto. Pia kuwahimiza wanawake kuzingatia chanjo na tiba zote wakati wa uja uzito.
Pia Mkuu wa Wilaya ametoa wito wa wataalam wa afya wawafundishe wamama wajawazito na wananchi kwa ujumla ili kuandaa na kupata lishe bora kama mbogamboga, mayai, na matunda ambazo zinapatikana katika mazingira yao na kwa bei nafuu.
Katika Sherehe hizi za Siku ya Wanawake Dunia Mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri. Katika siku hiyo Wanawake wamechangiwa zaidi ya Shilingi Milioni Mbili (Tsh. 2,000,000/=) zimepatikana kwa ajili ya kutunisha mfuko wa wanawake ambazo zilichangwa kwa harambee iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa. Pia wanawake hao wamefanikiwa kufungua akaunti katika Benki ya NMB.
Mkuu wa Wilaya amempongeza Dada Lucy Mdam (mlemavu wa macho) ambaye ni Afisa Maeleo ya Jamii katika kitengo cha Walemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa kuimba shairi zuri lenye ujumbe mzito katika kila beti. Cha kushanga Dada Lucy Mdam ni mlemavu wa macho na haoini kabisa ila amegusa nyanja nyingi za maendeleo na kuwataka wanawake wabadili fikri zao ili waweze kujikomboa na kushika nafasi mbalimbali katika Taifa hili.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.