Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ambaye ndiye mgeni rasmi, Mhe. Jabir Shekimweni amefungua maadhimisho ya Siku ya Unyonyeshaji Dunia yaliyofanyika kiwilaya katika ukumbi wa kliniki ya watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa. Maadhimisho haya yamehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime, madaktari, wauguzi, wataalamu wengine, wazazi, wajawazito na wananchi kwa ujumla.
Siku ya Unyonyeshaji Duniani huadhimishwa kuanzia tarehe 1 Agosti mpaka 7 Agosti kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ni “UNYONYESHAJI WA, MAZIWA YA MAMA NI MSINGI WA MAISHA YA MTOTO”.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (aliyesimama) Akitoa Hotuba katika Siku ya Unyenyeshaji Dunia. (Picha na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Pia maadhimisho haya yameambatana na mafunzo ya jinsi ya kumnyonyesha mtoto toka anapozaliwa hadi kufika umri wa miaka miwili. Akitoa mafunzo haya Bi.Petronida Mahanyila ambaye ni Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto amesema "Mtoto anapozaliwa anatakiwa kunyonyeshwa kwa muda wa miezi sita mfululizo bila kumlisha vyakula vingine, na baada ya miezi sita anatakiwa kuendeleakukunyonyeshwa kwa muda wa miaka miwili sawa na siku 1000 huku akichanganyiwa vyakula laini kama vile uji wa nafaka wenye virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mtoto, juisi za matunda na vyakula vingine vilivyosagwa na kuwa laini".
Vile vile ameongeza kuwa "mama mjamzito anapaswa kuhudhuria kliniki mara tu anapata mimba ili aweze kupatiwa kinga mbalimbali za kumlinda mtoto aliyetumboni tangu mama anapopata ujauzito hadi kujifungua, kinga hizo zinasaidia kuongeza damu ya mama, kuzuia mtoto kuzaliwa akiwa na kasoro kama za mgongo wazi, mdomo kuchanika, kutopata maambukizi toka kwa mama, kumlinda mama na magonjwa mbalimbali"
Bi.Petronida Mahanyila ambaye ni Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto (aliyesimama) Akitoa Mafunzo ya Unyonyeshaji wa Mtoto na lishe bora kwa Mama na Mtoto katika Siku ya Unyenyeshaji Dunia. (Picha na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Katika hotuba yake mgeni rasmi amewaasa wajawazito kujifungulia hospitalini na sio kujifungulia nyumbani kwa kuwa kujifungulia hospitalini mama na mtoto anakuwa katika ungalizi salama kwa kupata matibabu na ushauri wa ukuaji wa mtoto. Pia ameongeza kuwa wazazi wanatakiwa kuwanyonyesha watoto wao kwa kuwa maziwa ya mama yana virutumisho vyote ambavyo vinamjenga mtoto kiakili na hivyo kupata watoto wenye akili nzuri na afya bora.
Pia ameeleza kuwa kumnyonyesha mtoto kwa muda wa miaka miwili kunasaidia kupunguza uwezekana wa kupata saratani ya matiti kwa kuwa maziwa yafanya mrundikano wa katika matiti na mwisho wa siku mama anweza akapata saratani ya matiti.
Vile vile amesisitiza kuwa wazazi watumie uzazi wa mpango ili kupata watoto kwa wakati na kwa nafasi hii inasaidia kupata watoto wenye afya bora na wazazi kuweza kuwapatia mahitaji muhimu.
Wazazi wakisikiliza kwa Umakini Hotuba ya Mgeni Rasmi Ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri katika Siku ya Unyenyeshaji Dunia. (Picha na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Baada ya kutoa hotuba hiyo Mgeni rasmi ametoa zawadi ya sabuni ya unga yenye ujazo wa kilogram moja kwa kila mzazi na mjamzito. Hivyo wazazi wamempongeza sana Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri kwa msaada huo na nasaa zake, na wameahidi kutekeleza mambo yote ya muhimu katika ukuaji wa watoto wao.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (aliyesimama) Akitoa Zawadi ya Sabuni ya Unga Kilogram Moja kwa Kila Mama Mjamzito na Mzazi katika Siku ya Unyenyeshaji Dunia. (Picha na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Kwa taarifa zaidi juu ya taarifa Hii pakua Nyaraka hii hapa chini:
Risala kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa katika Siku ya Unyonyeshaji Duniani.pdf
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.