Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Shirika la AM-FM na Asasi ya Kiraia Tanzania Youth Alliance (TAYOA) leo imetambulisha program maalam ya kuwakinga wasichana waliobalehe na wanawake vijana ndani na nje ya shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Katika warsha hii ya siku moja imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo waheshimiwa madiwani ambao ni wenye viti wa kamati za kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, wakuu wa idara za afya, elimu, maendeleo ya jamii, mipango na takwimu, viongozi wa dini na Asasi za Kiraia. Aidha warsha hii imefunguliwa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa Ndg. Apolonia Temu akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Mussa Shekimweri na kufungwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Mhe. Joctan Cheligah ambaye ni diwani wa kata ya Lumuma akimwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Donath Nghwenzi ambaye pia ni diwani wa kata ya Massa. Pia warsha hii imehudhuriwa na Ndg. Khamlo Njovu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Mpwapwa Ndg. Maria Leshalu.
Wakuu wa idara, waheshimiwa madiwani na wadau wengine wakifuatilia warsha ya kuwakinga wasichana (kulia mbele ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Dkt. Said Mawji). ( Picha na Dkt. Said Mawji, Mganga Mkuu - Wilaya ya Mpwapwa).
Program hii ni ya majaribio na itatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika mikoa mitatu tu Tanzania Bara, mikoa hiyo ni Singida, Morogoro na Dodoma. Pia itashirisha halmashauri za wilaya kumi (10) za miko hiyo ambapo kwa mkoa wa Dodoma wilaya za Mpwapwa, Bahi, kongwa na Kondoa zimeteuliwa kwenye program hii.
Mhe. Joctan Cheligah (katikati) akifunga warsha hiyo, (kulia) Ndg. Khamlo Njovu, mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na (kushoto) Ndg. Emmanuel mkuu wa msafara toka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.(Picha na: Dkt. Said Mawji - Mganga Mkuu Wilaya ya Mpwapwa)
Mtaalam toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg. Emmanuel, amesema kuwa program hii inawalenga hasa wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walioko kwenye mpango wa kaya masikini katika vijiji 57 vilivyopo wilaya ya Mpwapwa. Lengo likiwa ni kuwawezesha kujitambua, kujikinga na mihemko inayosababishwa na mabadiliko ya mwili katika ukuaji.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.