(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 Ndugu. Mzee Mkongea Ali leo ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Wodi ya Utapiamlo Mkali inayojengwa katika eneo la Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa. Jengo hilo limefadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Action Against Hunger.
Aidha katika taarifa iliyowasilishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya Ndugu. Achard Rwezaula inasema "Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ina jumla ya watoto 70,117 ambao wapo chini ya miaka mitano, lakini 37% ya watoto wana Udumavu lakini takwimu pia zinaonesha kuwa watoto wenye uzito pungufu ni asilimia 12, wakondefu ni 1% wenye upungufu wa damu ni asilimia 30. Hali hii ni mbaya na inahitaji nguvu kubwa ielekezwe kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto wetu ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa la kesho".
Hali ya lishe ya wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 15-49) nayo bado ni mbaya; sote tunajua, hali ya lishe ya mama ikiwa mbaya inaathiri hali ya mtoto toka tumboni pamoja na malezi na makuzi ya mtoto.
Tafiti za hivi karibuni zimebaini kwamba, kati ya wanawake kumi, wastani wa wawili wana utapiamlo. Lishe duni kwa wanawake wajawazito inachochea hatari ya kujifungua watoto njiti, waliodumaa au kuharibu mimba. Asilimia 02 ya wanawake wa Mpwapwa walio katika umri wa kuzaa wana upungufu wa damu. Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi wakati au baada ya kujifungua.
Vifo vya wanawake wajawazito vitapungua sana endapo Serikali kwa kushirikiana na Wadau tutakuwa na mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto mbalimbali zinazomkabili mama mjamzito, aliyejifungua na mtoto chini ya miaka mitano.
Pia ndani ya Halmashauri kuna miradi miwili inayojihusisha na shughuli za Lishe moja kwa moja, nayo ni Action Against Hunger wanaojihusisha na kupunguza Utapiamlo Mkali (IMAM) na Lishe Endelevu wanaojihusisha pia na Lishe kwa kuwaongezea uelewa jamii ya mambo yahusuyo Lishe.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na mama wajawazito kutohudhuria Kiliniki au kuchelewa kuanza kiliniki wakati wa ujauzito, kujifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi ambao hawana utaalam, kukosa mahitaji ya msingi kama vile chakula, muda wa kupumzika, ulishaji wa watoto wachanga na wadogo usiozingatia kanuni na taratibu; hizi ni baadhi tu ya changamoto zinaathiri lishe na afya ya mama na mtoto.
Serikali kupitia Halmashauri ya WIlaya ya Mpwapwa inaendeleo kutoa matone ya Vitamini A na dawa za minyoo na kupima hali ya Lishe. Takwimu zinaonyesha Halmashauri ina watoto wa miezi (6-59) 59599 na kati ya hao waliopewa matone ya Vitamin A na dawa za minyoo na kupimwa hali ya Lishe ni 56599 sawa na 94%. Lakini kwa robo hii ya nne wanawake wajawazito waliopewa vidonge vya madini joto ni 11570 kati wanawake 12018 ya waliofika kliniki sawa na 96%.
Kwa kuona umuhimu huo na hali ilivyo katika Wilaya ya Mpwapwa, ndio maana Action Against Hunger wamekuja na Mradi wa Kujenga Wodi maalum itakayohudumia watoto wenye utapiamlo mkali. Fedha iliyolengwa ili kukamilisha Ujenzi wa Kituo cha matibabu ya Utapiamlo Mkali ni Tshs. 130,480,586.00. Kiasi cha fedha ambacho AAH imetoa kwa ajili ya ujenzi kufanikisha ujenzi huu hadi sasa ni Tshs. 123,887,398.70. Bado awamu ya mwisho ambayo ni sawa Tshs. 6,524,029.30. Hadi sasa fedha iliyotumika kwa ajili ya ujenzi na vifaa ni Tshs. 100,089,158.00 na fedha iliyobaki kwenye akaunti ni Tshs.23, 887,398.70. Jengo lipo kwenye hatua za mwisho katika kufunga madirisha na kuweka mfumo wa maji ndani ya wodi.
Pia kuna changamoto ya matumizi ya chumvi yenye madini joto. Tulikusanya sampuli 30 za chumvi kutoka kwenye baadhi ya kaya hapa mjini Mpwapwa kwa kutokubagua, baada ya kupima sampuli 26 zilikuwa na madini joto sawa na 87% na sampuli 4% hazikuwa na madini joto sawa na 13%.
Pia tulichukua sampuli 6 kutoka kwenye maeneo wanakozalisha chumvi hapo Godegode, sampuli 5 hazikuwa na madini joto sawa na 83% na sampuli 1 sawa na 17% haikuwa na madini joto. Mama mjamzito anapotumia chumvi isiyo na madini joto; afya ya mtoto inaathirika sana kwani anaweza kuzaliwa akiwa na udumavu wa ubongo au ulemavu wa viungo. Pamoja na jitihada za sekta mbalimbali mtambuka katika kuboresha hali ya lishe hapa wilayani, bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu ya pamoja ili kuifikia jamii na hasa kipengele cha kubadili tabia.
Hali ya usafi wa madhingira na matumizi ya choo katika wilaya ya Mpwapwa sio ya kuridhisha sana hii ni kwa kuwa bado jamii zetu hazioni umuhimu wa kuwa na vyoo lakini pia hazitumii sabuni wakati wa kunawa mikono hasa baada ya kutoka chooni na kabla ya kula chakula, hali hii inasababisha magonjwa ya milipuko ambayo yanatumia gharama kubwa kuyatibu kama magonjwa ya kuhara, minyoo, magonjwa ya macho na ngozi. Baadhi ya magonjwa haya haswa yanapokuwa sugu yanapelekea watoto kupata utapiamlo ikiwa ni pamoja na udumavu wa kimwili na kiakili. Kwa takwimu zilizokusanywa robo ya nne zinaonesha kaya 25474 zina vyoo bora kati ya kaya 70129 sawa na 36%. Lakini kaya 14483 sawa na 21% kati ya 70129 hawana vibuyu chirizi vya kunawia mikono punde wakitoka chooni.
Hata hivyo, hali ya Matibabu ya Utapiamlo kwenye hospitali ya Wilaya na vituo vya kutolea huduma za Afya ni kama ifuatavyo watoto 485 walio chini ya miaka mitano walikuwa na Utapiamlo Mkali kwa robo ya tatu, robo hii ya nne watoto tulipata wagonjwa wapya 230, kati ya hao wagonjwa wapya ni 167 wametibiwa na kurudi majumbani kwao. Lakini watoto 75 wamekimbia (defaulters) matibabu na watoto 4 walifariki ni kwa sababu walicheleshwa kufikishwa kwenye matibabu mapema.
Pia watoto 449 wanaendelea na matibabu ya Utapiamlo Mkali katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za Afya kwenye robo hii ya kwanza kwa mwaka 2019/20.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.