(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo amezindua Dhahabu ya Kijani katika shamba la Chuo cha Ualimu Mpwapwa. Uzinduzi huo umehudhuriawa na Waheshimiwa madiwani, kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mpwapwa, Wakuu wa Idara na taasisi, vikundi vya wakulima na wananchi kwa ujumla.
Dhahabu ya Kijani ni jina lililopata maafuru la zao la Korosho kwa kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara, kutokana na manufaa hayo Wilaya ya Mpwapwa imeamua Zao hilo kulifananisha na Dhahabu na hivyo kiliita kwa jina la Dhahabu ya Kijani. Katika uzindizi wa zao hilo la Korosho umeambatana na shughuli za utoaji wa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla juu ya namna ya kuandaa shamba la korosho, namna ya kupanda, kupalilia na kuweka dawa za kuua wadudu waharibifu wa zao hilo, kuvuna pamoja na kuelezewa faida ya zao la korosho ikiwemo kupata faida ya fedha, chakula, dawa, sharubati (juice) na viungo vya mboga. Elimu hiyo ya kilimo cha Korosho imetolewa na mtaalam wa kilimo toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Edson Kileo ambaye pia ndio msimamizi na mshauri wa kilimo cha korosho katika Wilaya ya Mpwapwa. Pia mtaalam huyo wa kilimo ameahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha wakulima wote wa kilimo cha korosho kwa kutembelea mashamba yao na kuwa ushauri kitaalam katika kutatua changamoto zao.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri Akitoa Hotuba kwa wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria katika siku ya Uzinduzi wa Upandaji wa Mikorosho katika Shamba ya Chuo cha Ualimu Mpwapwa tarehe 10 Disemba, 2018.
Zao la Korosho lilianza kuwekewa mkazo wa kulimwa Mpwapwa tangu Mwaka 2017 na limeonyesha matumaini mazuri ya kustawi vizuri katika Maeneo ya Chunyu, Nghambi, Mazae, Lupeta na Ilolo, ambapo wakulima wa maeneo hayo miche yao ya mikorosho inakua vizuri. Pia wataalam wa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa Kushirikiana na Wataalam toka Chuo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele cha Mtwara wanaendelea kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mpwapwa ili zao hilo lenye tija na mafanikio makubwa kuweza kulimwa maeneo mengi ya Wilaya ya Mpwapwa.
Mtaalam wa kilimo cha zao la korosho Ndug. Edson Kileo akitoa elimu juu ya upandaji wa mche wa mkorosho katika shamba la Chuo cha Ualimu Mpwapwa katika siku ya uzinduzi wa Upandaji wa zao la korosho Wilayani Mpwapwa.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amezindua kauli mbiu yenye maudhui ya kuwahamasisha wananchi na wadau mbalimbali kuwekeza katika shughuli za kiuchumi ili kuweza kuinua kipato na kujenga uchumi imara wa Wilayani Mpwapwa. Kauli mbiu hiyo ni "Inuka, Tuijenge Mpwapwa Mpya". Ujumbe huu umeandikwa kwenye bango kubwa na katika T-Shirt zilizovaliwa na washiriki waliohudhuria katika Uzinduzi wa Upandaji wa Zao la Korosho uliofanyika katika shamba la Chuo cha Ualimu Mpwapwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wanne kushoto) Akiwa katika Picha ya Pamoja na kamati ya ulinzi na pamoja na wakuu wa idara Mara baada ya Kuzindua Upandaji wa Mikorosho katika Siku ya Uzinduzi wa zao la Korosho katika Shamba ya Chuo cha Ualimu Mpwapwa tarehe 10 Disemba, 2018.
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ameziagiza taasisi zote zilizopo katika Halmashauri ya Mpwapwa kuwa na Mashamba ya Korosho ili kuwahamasisha wananchi kuwa na mwamko wa kulima zao hilo na baadae kunufaika na faida zake. Pia, amewaagiza wakuu wa idara na taasisi angalau kila mmoja kuwa na ekari moja la shamba la korosho kwa kuwa mashamba bado yapo ya kutosha hivyo hakuna sababu ya mtu kukosa shamba.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri Akitoa Hotuba kwa wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria katika Uzinduzi wa Upandaji wa Mikorosho katika Siku ya Uzinduzi wa zao hilo katika Shamba ya Chuo cha Ualimu Mpwapwa tarehe 10 Disemba, 2018.
Sambamba na hilo Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri, amewataka wananchi wote kuandaa mashamba ya kupanda mazao ya chakula ili kuondokana na janga la njaa.
Kwa upande wao wananchi walihudhuria wamempongeza sana Mkuu wa Wilaya kwa kuwaletea kilimo cha Korosho na kugawa miche bure kwa wakulima, hivyo wameahidi kuwa
wataitunza miche vizuri kwa kufuata kanuni za kilimo cha korosho kama walivyoelekezwa na mtaalam wa kilimo cha Korosho wa Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Edson Kileo.
Mtaalam wa kilimo cha zao la korosho Ndug. Edson Kileo akitoa elimu ya upandaji wa mche wa mkorosho kwa vitendo katika shamba la Chuo cha Ualimu Mpwapwa katika siku ya uzinduzi wa upandaji wa zao la korosho Wilayani Mpwapwa.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.