(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imekuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, kwa asilimia 111 mpaka kufikia mwezi Mei 2019 baada ya Halmashauri ya Kondoa Mji ambayo ni ya kwanza kufika lengo. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul M. Sweya katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Hii ina maana kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imekusanya mapato yake yote iliyotarajiwa kukusanya kwa asilimia 100 na kuongeza ziada ya mapato ya asilimia 11. Ambapo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ilikadiria kukusanya Bilioni 1.7 kwa mapato ya ndani, na hivyo kufanikiwa kukusanya kiasi hicho chote na ziada ya asilimia 11.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amemtaka Mkurugeniz wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kupeleka asilimia 20 kwa kila kijiji, asilimia 10 kwa wanawake, na vijana. Pia ameagiza kulipa posho zote za waheshimiwa madiwani kwa wakati kwa kuwa hakuna sababu ya kutolipa kwa kuwa tumevuka lengo letu la mwaka 2018/2019 ya makusanyo katika mapato ya ndani.
Aidha Mhe. Shekimweri ameipongeza menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa kushirikiana pamoja katika jitihada za kukusanya mapato kwa kuweka doria usiku na mchana katika vyanzo vyote vya mapato, kuwapiga faini wafanyabiashara walikuwa wanakwepa kulipa ushuru mpaka kufikia lengo hili.
Mhe. Shekimweri, amewaomba waheshimiwa madiwani kuwashawishi wananchi hususan wajasiriamali ili waweze kununua vitambulisho vya mjasiriamali, kujitokeza katika kushiriki katika shughuli za maendeleo kama kujenga miradi iliyopo katika kata zetu kama vile madarasa, maabara na vituo vya kutolea huduma ya afya. Pia amemuomba Meneja wa TARURA kuweza kuziingiza barabara zote za korofi zilizopo katika kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuziingiza katika Mpango kazi wake ili ziweze kutengenezwa na hatimae wananchi waweze kupata huduma za barabara hizo.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Shekimweri amewaomba waheshimiwa madiwani pamoja na wananchi kwa ujumla kuweza kujitokeza kwa wingi katika Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 na kuchangia michango ili kufanikisha sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti 2019 katika Wilaya ya Mpwapwa.
Pia Mkuu wa Wilaya Mhe. Shekimweri amewashauri Waheshimiwa madiwani kufanya jitihada za kuupa uwezo Mji wetu wa Mpwapwa ili kuharakiwasha maendeleo ya Mpwapwa kwa kuwa tutapata wakurugenzi wawili na huduma za jamii zitaongezwa na kuwafikia wananchi kwa wakati.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.