Wilaya ya Mpwapwa ni miongoni mwa Wilaya za Nchini Tanzania zilizoshiriki zoezi la Kampeni ya Kutoa chanjo ya magonjwa ya Surua, rubella na Polio ya sindano kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Zoezi hilo lilizinduliwa kitaifa tarehe 17/10/2019 na kufanyika kwa muda wa siku 5 yaani kuanzia tarehe 17/10/2019 hadi 21/10/2019. Katika kutoa chanjo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliweka lengo la kitaifa katika utoaji wa chanjo hiyo kuwa kila wilaya ifikie 95% ya utoaji wa chanjo hiyo.
Kwa Wilaya ya Mpwapwa ilikuwa na watoto walengwa wa chanjo ya surua - rubella 55,603 na polio ya sindano ni 26,538, waliotarajiwa kupata chanjo hizo.
Baada ya kampeni ya chanjo hiyo kumalizika, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Chanjo Wilaya ameamua kuitisha kikao cha kutathmini zoezi la chanjo jinsi lilivyoendeshwa ili kubaini mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto kwa wakati ujao wa zezi kama hili. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Wilaya na kuhudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wajumbe wa Kamati ya Chanjo, Wakuu wa Idara na Viongozi wa dini.
Wajumbe wa Kamati ya Kampeni ya Chanjo wakiwa katika Kikao cha Tathmini ya Chanjo ya Surua, Rubella na Polio ya Sindano
Akiwasilisha taarifa ya tathmini ya chanjo hiyo Ndugu. Frugence Temu ambaye ni Mratibu wa Chanjo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa amesema "Katika kutekeleza zoezi la chanjo, tulipata changamoto nyingi kama vile baadhi ya maeneo kutofikika kwa wakati kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha hasa kata za milimani mfano: Lufu, Galigali, Mbuga, Wotta na Manghaliza. Pia baadhi ya magari yaliyopangiwa shughuli ya chanjo kutopatikana kutokana na mwingiliano wa shughuli zingine za kitaifa kama uchaguzi na mitihani ya kidato cha nne, na fedha kuchelewa kufika hivyo washiriki wa zoezi hilo walifanyakazi ya kizalendo kwa muda wote wa chanjo bila kulipwa, na walilipwa baada ya zoezi kuisha". Temu ameongeza kuwa "japo kulikuwa na changamoto zote hizo lakini Wilaya ya Mpwapwa ilifanikiwa kuchanja chanjo ya surua-rubella watoto 56,726 sawa na 102% na polio ya sindano 27,567 sawa na 104% na hivyo kufanikiwa kuvuka lengo la kitaifa la kuchanja 95%."
Wajumbe wa Kamati ya Kampeni ya Chanjo wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri (katikakati) mara baada ya kumaliza Kikao cha Tathmini ya Chanjo ya Surua, Rubella na Polio ya Sindano.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amewapongeza washiriki pamoja na wajumbe wa kampeni ya chanjo kwa kufanikisha zoezi hili kizalendo kabisa, huku akitoa wito namna zeozi hili lilivyotekelezwa iwe hivyo kwa shughuli zote za kitaifa na kiwilaya. Vile vile Mhe. Shekimweri ameongeza kuwa "nilipata taarifa kuwa baada ya kuona watu wengi hawajitokezi katika vituo vilivyoanishwa ili kupata chanjo mliamua kuwatembelea nyumba kwa nyumba ili kuwafikia walengwa wote, kwa jitihada hizi za kizalendo nawapongeza sana".
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa ametumia fursa hii kuwaonya watumishi wa uuma kutojiingiza katika mambo ya siasa au kutoa huduma kwa wananchi kwa misingi ya upendeleo wa chama cha siasa. Mtumishi atakayebainika kufanya hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.