(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imepata mradi mpya wa Kuongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kutoka kwa wafadhili ya Nchi ya Finland kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huo umetambulishwa katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ukiwa umehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri, Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambaye ni Diwani wa Kata ya Mpwapwa Mjini Mhe. George Fuime, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpwapwa Ndugu. Paul M. Sweya, Waheshimiwa madiwani, Wakuu wa idara na Maafisa Tarafa. Mradi huo unajulikana kwa jina la "PROGRAMU YA KUENDELEZA MNYORORO WA THAMANI WA MAZAO YA MISITU (FORVAC)".
Mradi huo umelenga kutekelezwa katika Mkoa wa Dodoma na ni wilaya moja tu ya Mpwapwa kwakuwa bado maeneo mengi ya misitu hayajaathiriwa na shughuli za binadam. Katika Wilaya ya Mpwapwa umelenga kuhudumia vijiji sita ambavyo ni: Lwihomelo kata ya Wotta, Chiseyu kata ya Gulwe, Chitemo kata ya Chitemo, Nduga kata ya Mlembule, Ikuyu kata ya Luhundwa na Lufusi kata ya Lumuma.
Lengo kuu la program hii ni Kuongeza faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu. Mradi huu wa FORVAC Chimbuko lake limetokana na programu zilizopita za Ushirikiano wa baina ya Serikali za Tanzania na Finland, kama vile National Forest and Beekeeping Programme (NFBKP II, 2013–2016) & Lindi and Mtwara, Agribusiness Support (LIMAS, 2010–2016) ambao Ulisaidia usimamizi endelevu wa misitu – PFM na Kuzalisha kipato na ajira kwa wananchi kutokana na misitu ya vijiji.
Pia kulikuwa na program zingine kama Private Forestry Programme Private Forestry Programme (PFP, 2014–2018) Panda miti kibiashara: iliwezesha Kuendeleza mnyororo wa thamani, Kuhamasisha wananchi kujihusisha na shughuli za kiuchumi na Kuendeleza mafunzo na huduma za ughani kwa wakulima wadogo wa mashamba ya miti.
Hivyo mradi huu wa Kuendeleza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) umeangalia mafunzo yaliyopatikana na shughuli chanya kutokana na miradi iliyopita ikiwa pamoja na maeneo ya miradi iliyopita.
Katika mradi huu wa FORVAC kunatarajiwa matokeo ya Kuboreka kwa mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye sekta ya misitu, Kuongezeka kwa uwezo wa wadau katika kuhamasisha na kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, Uwepo kwa mfumo mathubuti wa huduma za ugani, mawasiliano na ufuatialiji wa shughuli za programu na Uwepo wa sera na sheria wezeshi za kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na usimamizi endelevu wa misitu.
Katika kutekeleza mradi huu masuala mtambuka ya kuzingatiwa yameainishwa kama vile Haki sawa katika kutekeleza mradi ukizingatia: Uwazi & Uwajibikaji (utawala bora), kujituma na kupata matokeo, Kuwa na uwazi na shirikishi, Kuhusisha makundi yote katika jamii na hata wasiojiweza, Haki ya kushiriki katika utoaji wa maamuzi, utumiaji na kugawana faida kutokana na maliasili ya misitu sawa (Right to participate in decision making, utilisation and benefit sharing of forest resources), Wananchi ndiyo wenye haki na wajibu wa kubeba majukumu ya kusimamia maliasili (Rights holders & Duty bearers), Kuhamasisha wanawake kushiriki katika mafunzo ya kuongeza ujuzi wa biashara na shughuli za kuongeza kipato, Kuzingatia usawa kwa jinsia zote na Kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mbinu stahiki.
Pia Mrati wa mradi wa FORVAC Ndugu.Ndugu. Petro Masolwa ameelezea namna mazoa ya misitu yatakavyoongezwa thamani kama vile mbao zitatengenezwa fanicha, magogo yatatengenezwa mbao, asali itawekwa katika vifungashio maalum pia kutengeneza inta, na utengenezaji wa ceilling board kutokana na mabaki ya mbao zilizolandwa. Vilevile ameongeza kuwa mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye sekta ya misitu utaboreka na Kuboresha mnyororo wa thamani ya mazao misitu, makuu kama mbao, mkaa, asali, Uyoga na Matunda pori.
Aidha Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Fuime amesema kwa niaba ya wajumbe wa mkutano huu wa utambulishaji wa mradi wa FORVAC katika wilaya ya Mpwapwa wameupokea mradi huu na kuhaidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wake ila wameomba elimu zaidi itolewe kwa wananchi na ushirikishwaji ufanyike kwa vijiji vya mradi na vile vinavyopakana na vijiji vya mradi ili kuwa na uwelewa wa pamoja. Vile vile Mhe. Fuime ameongeza kuwa "hapo awali kulikuwa na program ya Utunzaji wa Misitu (HADO) ambapo Dodoma ilifanya vizuri sana na mpaka sasa unaona misitu hii". Hivyo program hii itafanikiwa hapa Mpwapwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amemuomba Mratibu wa Mradi wa FORVAC Ndugu. Petro Masolwa kuongeza vijiji vingine vya mradi angalau kufikia vijiji 20 hivi maana vijiji sita ni vichache kati ya vijiji 113 vya Halmashuri ya Wilaya ya Mpwapwa. Pia amesisitiza kuwa ateuliwe mtaalam mahsusi (focal person) kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa ajili ya usimamizi wa karibu wa mradi huu na atakuwa anaandaa taarifa zote za mradi.
Wajumbe wote waliohudhuria mkutano huo kwa pamoja wameupokea mradi huo na wamehaidi kushirikiana na wataalam katika utekelezaji wake.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.