(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amefunguo kikao cha utambulisho wa Mradi wa Kuthibiti Magonjwa ya Milipuko hususani kipindupindu, mradi huu unajulikana kama Majirani Wema (Good Neighbours). Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa kuhusisha Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Paul Mamba Sweya pamoja na wakuu wa idara wote.
Katika utambulisho wa Mradi huu imeelezwa kuwa Mkoa wa Dodoma kuanzia mwaka 2016 mpaka mwaka 2018 kila mwaka ulikuwa na mlolongo wa kipindupindu katika wilaya zote za Dodoma, na kwa Wilaya ya Mpwapwa ndio kulikuwa na wagonjwa wengi wa kipindupindu. Kila mwaka ifikapo mwezi wa Septemba mpaka Januari kulikuwa na wagonjwa wa kipindupindu zaidi ya 600 katika Mkoa mzima wa Dodoma, kwa Mpwapwa peke yake zaidi ya watu 300 walipwa na kipindupindu na 16 kati ya hao walifariki dunia.
Wakuu wa idara akiwa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kusikiliza utambulisho wa Maradi wa Good Neighbours
Mwakilishi wa mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema, "Katika vituo vya afya 10 nilivyopitia tuliona magonjwa makuu ni kuharisha na hivyo inaonyesha hakuna usafi thabiti katika maeneo yetu". Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia Program ya Ubadilishaji wa Tabia kwa Wananchi, (Behavour Change Communication - BCC) katika kuchimba visima vya maji na kuchimba vyoo. Mpwapwa ndio ya kwanza kwa kuanzishwa kwa mradi wa kuthibiti Kipindupindu kabla hakijatokea, na haijawahi kufanyika popote Nchini.
Pia imeelezwa kuwa mwaka huu 2019 hakuna mgonjwa yoyote wa kipindupindu ameripitiwa katika Mkoa wetu, hii ni kutokana na juhudi mbalimbali zilizowekwa na mkoa ikiwemo na usafi wa mazingira, kufuata kanuni za afya, kuhamasisha wananchi kuwa na vyoo bora.
Mradi huu wa kuthibiti ugonjwa wa kipindupindu unafadhiriwa na Shirika la Majirani Wema (Good Neighbour) na watatumia program ya BCC kwa maana ya kuwashirikisha wananchi kuhitaji vipaumbele vyao ili miradi iwe endelevu. Miongoni mwa mambo ambayo mradi utafanya kuhakikisha kipindupindu hakitokei tena na pamoja kujenga vyoo vya bora na vya kisasa, kuchimba visima vya maji safi na salama na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kanuni za afya.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amesema, "Sababu kubwa ya kuwa na kipindupindu kutokuwa na vyoo bora na changamoto ya maji, ambapo Serikali imejitahidi kutekeleza miradi ya maji katika Wilaya ya Mpwapwa na tuna miradi 10 ya maji kati ya hiyo miradi 7 ni mipya yenye thamani ya Tsh 4.3 bilioni, pia kuna miradi ya visima vifupi na tunafanya utafiti katika miradi 18 ya maji ya visima imefanyiwa upembuzi yakinifu kwa mwaka huu 2018/2019, hivyo ujio wa mradi huu utatuongezea nguvu.
Mwezeshaji wa Mradi wa Good Neighbours akitoa utambulisho wa mradi kwa Wakuu wa idara katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Pia Serikali imekuwa ikitoa matamko mbalimbali ikiwemo kila kaya kuwa na choo bora ifikapo tarehe 31 Desemba 2019, kwa sasa kwa tathimini ya Wilaya ya Mpwapwa mpaka Novemba mwaka 2018 kulikuwa na kaya 3,330 kati ya kaya 80,000 hivi hazina vyoo bora sawa na 4%, baada ya jitihada kubwa hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu ni kaya 1,400 hazikuwa na vyoo baadhi ya maenneo hayo ni Mpwapwa Mjini na Godegode. Ila kwa sasa idadi ya kaya zisizo na vyoo imepungua mpaka na tumeweka mikakati na muda maalam mpaka kufikia mwezi Machi 30, 2019 kaya zote zisizo na vyoo kuwa na vyoo bora.
"Nimeanzisha kampeni ya wataalam, maafisa watendaji wa kata na vijiji kupita kila kaya kukagua vyoo na kwa wale wasio na vyoo wahamasishwe kujenga vyoo na kila wiki napata taarifa juu ya zoezi hili, pia maelekezo ya mkoa yanasema baada ya wananchi kuvuna mazao basi watumie muda huo kujenga vyoo bora kwa kuwa watakuwa na kipato. Hivyo nawashukuru sana wafadhiri wetu Good Neighbours kuliona hilo na kuja kutusaidia ili kutokomeza magonjwa ya Mlipuko na kwa niaba ya wananchi wa Mpwapwa nawakaribisha na niwahakikishie ushirikiano mkubwa miongoni mwetu kama viongozi na wananchi kwa ujumla".
Mkuu wa Wilaya ya mpwapwa (wapili kushoto) akiwa na wajumbe waliohudhuria katika utambulisho wa mradi wa Kuthibiti Kipindupindu unafadhariwa na Good Neighbours
Kwa upande wao Majirani Wema (Good Neighbours) wamesema vijiji vya Wilaya ya Mpwapwa vitakavyofaidika na mradi huu ni vinne navyo ni; Chamanda, Igoji II, Muungano na Njiapanda. Miongoni mwa fursa hizo ni kuchimba visima vya maji, kujenga vyoo bora na kutoa elimu ya kanuni za afya. Hivyo wametoa wito kwa wananchi kujitolea maeneo yao kwa ajili ya kuchimba visima vya maji. Pia wafadhiri wa mradi wa Majirani Wema wamesema pia watatoa elimu namna ya kuepuka magonjwa ya milipuko hususani kipindupindu kwa wanafunzi, wananchi na viongoozi wa maeneo hayo ili kuwa na matokeo chanya.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.