(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Binilith Mahenge leo amezindua rasmi Bima ya Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa kimkoa ambapo imefanyika katika Wilaya ya Mpwapwa. Uzinduzi huo umehudhuriwa na wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, wenyeviti wote wa Halmashauri za Wilaya za mkoa wa Dodoma na meya wa jiji la Dodoma, Makatibu tawala wote wa wilaya za mkoa wa Dodoma, wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya ya Mpwapwa, Mbunge wa jimbo la Mpwapwa, waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, waganga wakuu wa wilaya zote za Dodoma, Maafisa Maendeleo ya Jamii Wote wa Mkoa wa Dodoma, wafadhiri wa CHF toka mradi wa Tuimarishe Afya (HPSS) na wananchi kwa ujumla.
Meneja wa mradi wa HPSS Mkoa wa Dodoma unaofadhiri mradi wa Bima ya Afya ya CHF Bw. Gondwe (aliyesimama) akieleza sababu ya kuwa na CHF iliyoboreshwa Nchi nzima na kufanya uzinduzi wa kimkoa Wilayani Mpwapwa
Uzinduzi huo wa kimkoa umefanyika wilayani Mpwapwa kutoka na sababu kuu mbili, kwanza Wilaya ya Mpwapwa ni Wilaya iliyofanya vizuri katika kutoa huduma ya CHF iliyoboreshwa tangu kuanza kwake Mwezi Julai 2018 kuliko wilaya zote za Mkoa wa Dodoma ambayo mpaka leo imeandikisha kaya mpya 429. Pili historia ya kuanzishwa kwa CHF iliyobreshwa ilianzia Wilayani Mpwapwa katika Kata ya Kibakwe baada ya mwananchi mmoja alivyouliza swali kuwa "Kwa nini bima ya Afya ya CHF haitumiki Nchi nzima kama ilivyo kwa bima ya afya ya NHIF kwa sababu sisi wananchi tunasafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine?" Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuanza kufikiria kuboreshwa kwa bima ya CHF ambapo kwa sasa CHF imeboreshwa, kaya moja yenye watu sita hulipa Tsh. 30,000.00 na wanatibiwa katika hospitali yoyote yenye kutoa huduma ya bima ya afya Nchi nzima. Vile vile CHF iliyoboreshwa inatolewa ndani ya muda mfupi kama nusu saa tu mpaka mteja kupata kadi na kuanza kuitumia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kulia) akipata maelezo juu ya CHF iliyoboreshwa toka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa
Kwa Mkoa wa Dodoma ulianza kutekeleza shughuli za CHF tangu Julai mwaka 2012 ambapo mwanachana wa CHF alikuwa anachangia Tsh. 10,000.00 kwa watu sita kwa mwaka na walikuwa wanatibiwa ndani ya wilaya tu. Kwa sasa CHF iliyoboreshwa kwa mujibu wa waraka namba 1 wa Mfuko wa Maboresho ya afya ya Jamii (CHF) wa tarehe 6 Aprili 2018 ambao umeanza kutekelezwa tangu Mei 2018. Katika maboresho haya yamepelekea kupanda kwa gharama za matibabu na kuwa Tsh. 30,000.00 kwa kaya yenye watu 6 kwa mwaka na ukiwa na bima ya CHF iliyoboreshwa unaweza kutibiwa popote nchi nzima.
Katika zoezi hili la uzinduzi wa CHF iliyoboreshwa limeambatana na zoezi la Upimaji wa Virusi Vya UKIMWI na uandikishwaji wa Wanachama wapya wa CHF unaofanyika moja kwa moja papo kwa papo.
Wananchi wakiwa katika Viwanja vya stendi ya zamani Wilayani Mpwapwa wakifuatilia uzinduzi wa CHF iliyoboreshwa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Mahenge ameleza mambo mengi yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ndani ya miaka hii mitatu katika sekta ya afya, Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika mkoa wa Dodoma. Kwa mara ya kwanza Mkoa wa Dodoma umefanikiwa kuwa na vituo vya afya 22 vyenye huduma zote muhimu na vipo kila wilaya ambavyo ujenzi wa kila kituo unagharimu si chini ya Tsh. 500,000,000.00, kwa hivyo uzinduzi huu wa bima ya CHF iliyoboreshwa unafanyika wakati kukiwa na uhakika kuwa vituo vya afya vipo, pili katika Mkoa wa Dodoma Mhe. Rais Magufuli amehidhinisha fedha za ukarabati wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ukarabati wa Chuo cha Afya Mvumi umegharimu zaidi ya Tsh. 5,000,000,000.00, Ukarabati wa Chuo na Hospitali ya Milembe umegharimu zaidi ya Tsh. 4,000,000,000.00, amewezesha uwekezaji mkubwa unaofanyika katika hospitali ya Benjamin Mkapa pale UDOM na yenye vifaa vya kisasa kama MRI na CT Scan, nne, amehidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali nne za wilaya ya Chemba, Chamwino, Kondoa na Bahi si chini ya Tsh. 1,500,000,000.00 na ujenzi utaanza wakati wowote, hivyo tunaposema watu wajiunge na huduma ya CHF tunauhakika kuwa watapata huduma zote za afya. Tano, Mhe. Rais Magufuli ameagiza fedha zote Tsh. 995,182,000 zilizotakiwa kutumika katika Sherehe za Uhuru mwaka 2018 zitumike katika kujenga Hospitali itakayoitwa Uhuru Hospital mkoani Dodoma, sita, Mhe. Rais Magufuli ameongeza bajeti ya dawa kutoka Tsh. 900,000,000.00 hadi Tsh. 4,300,000,000.00 katika mkoa wa Dodoma na kwa sasa dawa zipo katika vituo vyote vya kutolea huduma ya afya.
Kikundi cha Ngoma cha Vijana wa Wilaya ya Mpwapwa wakitoa elimu kwa wananchi juu ya CHF iliyoboreshwa na kucheza kwa fimbo na moto kwenye vyungu vikiwa vichwani.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesema, Serikali imeweka malengo ya muda mrefu na mfupi kwa kila mwananchi kupata huduma ya afya kwa kutumia bima ili kupata huduma kwa bei nafuu, hasa waliopo katika sekta isiyo rasmi, malengo ya muda mrefu kila mwananchi ajiunge na bima ya afya na malengo ya muda mfupi ni kujiunga na bima ya CHF iliyoboreshwa ili kufikia lengo la Afya Bora kwa Wote. Tangu Julai 2012 hadi Juni 2018 mkoa wa Dodoma, idadi ya kaya waliyosajiliwa katika bima ya CHF ni 156,721 sawaa 35% ya kaya 447,773, ambapo kaya hai ni 29,345 amabazo zinaweza kupata huduma ya Afya. CHF iliyoboreshwa ilianza mkoa wa Dodoma Julai 2018 ambapo kila kaya inachangia Tsh.30,000.00 kwa mwaka na mafunzo kwa maafisa uandikishaji kwa kila kijiji yameshatolewa.
Katika kipindi cha kuanzia Julai mpaka 20 Novemba 2018 katika CHF iliyoboreshwa mkoa umesajili kaya 1,467zimesajiliwa katika Mfumo wa CHF iliyoboreshwa kwa ada ya Tsh. 30,000.00 ambapo Wilaya ya Mpwapwa 429, Dodoma Jiji kaya 380, Kongwa kaya 298, Chamwino kaya 101, Kondoa Mji 87, Kondoa 75, Chemba 55, na Bahi kaya 42. Hii inaonyesha kuwa kazi ya uandikishaji na uhamasishaji bado iko chini, hiyo natoa rahi kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge (aliyesimama) akihutubia wananchi wa Wilaya ya Mpwapwawa kwenye uzinduzi wa CHF iliyoboreshwa katika viwanja vya stendi ya zamani
Naziagiwa Agizo kwanza, kila wilaya ikafanye kampeni ya kuhamasisha wananchi kijiji kwa kijiji kujiunga na CHF iliyoboreshwa kwa gharama ya TSh. 30,000.00 kwa mwaka kwa kaya na wanapata uelewa wa kutosha juu ya CHF iliyoboreshwa ili wajiunge kwa wingi katika huduma hii. Pili, wakuregenzi watendaji kasimamieni kwa umakini shughuli za uhamasishaji na uandikishaji wa wananchi, na kila mwanachama taarifa zake zimewekwa katika mfumo wa IMIS na makusanyo ya fedha yanafanyika kwa mtandao (electronically). tatu, Fedha za wanachama wa CHF zinaingizwa katika akaunti ya CHF Mkoa kwa wakati na stakabadhi za kuwekea fedha benki ziwasilishwe kwa Katibu tawala mkoa kila mwisho wa mwezi, nne, fuatilieni kwa ukaribu huduma ya afya zinazotolewa kwa wanachama wa CHF iliyoboreshwa ili kama kuna changamoto zitatuliwe kwa wakati, tano, simamimieni kwa ukaribu na kuhakikisha kuwa suala la CHF linakuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vyote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mkoa, sita, wakurugenzi watendaji hakikisheni mnatenga fedha kupitia bajeti za Halmashauri kwa ajili ya kuhuisha kaya za wazee pamoja na kuchangia wazee ambao hawana kadi za huduma hii hadi sasa. saba, Waganga wa kuu wa Wilaya hakikisheni vituo vya kutolea huduma vinatumia fedha kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyopo, pia kusitokee kuwa kituo kina waganga ila hawapo vituoni, fuatilieni hili na nane wakurugenzi watendaji hakikisheni mnatumia bakaa la fedha za CHF hadi tarehe 30 Juni 2018 pamoja na fedha za tele kwa tele mnalipa madeni ya vituo vya huduma na kununua vifaa kwa ajili ya usajili wa wanachama wa CHF vinnunuliwa kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge (wa kwanza kushoto) akipata maelezo juu ya CHF iliyoboreshwa toka hatua ya kusajili mwanachama mpaka kupewa kadi
Aidha Dkt. Mahenge ameziagiza Halmashauri zote za kuhakikisha kuwa wakulima wanaandaa mashamba angalau kila mwanachi alime ekari mbili na wapande mzao yanayoendana na hali ya Dodoma kama mihogo, mtama, uwele, alizeti. Pia watu wasajiliwe katika daftari la wakulima ambapo kwa mwaka jana walisajiliwa wakulima karibu 3,000 na mwaka huu 2018 tutakuwa na wakulima zaidi ya hao.
Mwisho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewapongeza sana wananchi wa Mpwapwa kwa kuitikia kwa wingi katika kupata huduma ya Afya kupitia Bima ya CHF iliyoboreshwa na ametoa wito Halmashauri zote za mkoa wa Dodoma kuiga mfano wa Mpwapwa.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.