(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amefanya ziara katika kata ya Gulwe Wilayani Mpwapwa ambako Reli ya Treni ya Mwendokasi (SGR) inaendelea na ujenzi. Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa akiwa na viongozi wa mkoa na wa wilaya ya Mpwapwa amefanya mkutano na wafanyakazi na wasimamizi wa mradi huo wa SGR katika eneo la Gulwe. Katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa ameelezwa kuwa Ujenzi wa Reli ya Treni ya Mwendokasi (SGR) unaendelea vizuri na kasi yake inaridhisha na hivyo kwa kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa 376.5KM kitakamilika tarehe 25 Septemba 2021 kama makataba unavyosema.
Katika taarifa ya SGR iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Masanja K. Kadogosa, imeelezwa kuwa kutoka Morogoro hadi Makutupora kutajengwa stesheni 8, kati ya hizo kubwa zitakuwa 2 na 6 zitakuwa stesheni za kati. Stesheni kubwa zitajengwa katika maeneo ya Kilosa Mjini na Dodoma eneo la Kikuyu Kusini. Stesheni za kati zitajengwa maeneo ya Mkata, Kidete, Gulwe (Mpwapwa), Igandu, Bahi na Makutupora. Katika Wilaya ya Mpwapwa stesheni itajengwa eneo la Gulwe ambapo kwa sasa ujenzi unaendelea.
Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Mpwapwa kuchangamkia fursa zinazoletwa na mradi wa SGR kwa kuwa Gulwe itakuwa ni stesheni ya Treni ya Mwendokasi na hivyo kutakuwa na watu wengi toka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Nchi kuja Mpwapwa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kupitia treni. Hivyo amewataka wanachi kuwekeze katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula, kujenga nyumba bora na za kisasa za kulala wageni, kuwekeza katika hoteli na migahawa iliyoboreshwa, kufanya biashara na shughuli zingine halali.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amesema " Wananchi bado hawajalipwa fidia katika maeneo yanayopita reli katika Wilaya ya Mpwapwa ila nawapongeza wananchi wamekuwa waelewa na hawasimamishi shughuli za ujenzi wa reli kwa kuwa hawajapata fidia, kwa hiyo wamekuwa wazalendo". Pia, Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa Wilaya imejipanga kushiriki katika shughuli za kiuchumi kutokana na kuwepo kwa stesheni na reli, kama kuzalisha zao la korosho, alizeti, ufuta na kuanzisha mji wa viwanda katika eneo la Isinghu.
Aidha Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuregenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul Mamba Sweya kupima eneo la Isinghu na kupata vibali ili kuwa eneo la viwanda na viwanja vilivyopimwa ili kuweza kupanga mji na hivyo itapanua ukuaji wa mji wa Mpwapwa. Pia Mkuu wa Mkoa amepongeza maendeleo ya ujenzi wa reli unavyoendea kwa kasi na kwa ustadi mkubwa.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.