(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amezindua Kampeni Maalum ya Utoaji wa Chanjo ya Magonjwa ya Surua, Rubella na Polio ya sindano kwa watoto walio chini ya miaka mitano. Kampeni hii ni ya kitaifa ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imezinduliwa leo katika Viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa. Uzinduzi huo umehudhuriwa na wazazi wakiwa na watoto wao wenye sifa za kupata chanjo hizo. Pia wananchi pamoja na wakuu wa idara na taasisi wamehudhuria Uzinduzi huo kwa ajili ya kupata uelewa wa umuhimu wa chanjo hizo kwa jamii.
Wahudumu wa Afya Akiandaa dawa na vifaa tiba zitakazotumika katika zoezi la Uzinduzi wa Chanjo
Katika hotuba yake Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa imeeleza kuwa katika Wilaya ya Mpwapwa chanjo hiyo inatarajiwa kutolewa kwa watoto walio chini ya miaka mitano wapatao jumla yaoo ni 55,603 Surua - Rubella na 26,538 Polio.
Akiendelea kuhutubia Mhe. Shekimweri amesema " Wilaya ya Mpwapwa ni miongoni mwa wilaya zinazoshiriki zoezi la uendeshaji wa kampeni ya chanjo ya kitaifa za Surua, Rubella na Polio ya sindano kwa watoto chini ya miaka mitano (5)" . Pia ameongeza kuwa "Watoto wanaolengwa katika zoezi hili ni wale walio na umri kati ya miezi 9 hadi miezi 59 hawa watapatiwa chanjo ya Surua na idadi yao wapata watoto 55,603 na watoto wanaostahili kupata chanjo ya Polio ya sindano ni wenye umri kati ya miezi 18 hadi 42 (yaani mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu na nusu) ambao wapo 26,538".
Mkuu wa Wilaya amesisitiza kuwa asitokee mtu kuzuia watoto wasipate chanjo hii, pia utafiti umeonyesha kuwa kuna baadhi ya watoto hawapati chanjo hii husababishwa na wazazi wao kupuuzia tu. Pia kuna baadhi ya wagonjwa wa Surua na Rubella wapo majumbani lakini hawatolewi taarifa ili kupata tiba mapema. Hivyo ametoa wito kila mmoja kuwa balozi mzuri katika kampeni hii.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wapili kulia) Akishuhudia Mtoto Akipatiwa Chanjo.
Katika hotuba yake Mkuu wa Wilaya imeeleza kuwa; Chanjo hii inaanza leo tarehe 17/10/2019 hadi tarehe 21/10/2019 ambapo itachukua muda wa siku tano katika utekelezaji wake; na maeneo yatakayohusika na utoaji wa chanjo ni vituo vya kudumu ambavyo ni zahanati, Vituo vya afya, Hospitali na Vituo vya Kuhamahama hasa sehemu ambazo hakuna zahanati inaweza kutolewa kwenye ofisi za shule, kijiji, sokoni au Godown kadri ya mazingira yatavyoruhusu ili kuhakikisha kila mlengwa amefikiwa.
Akiwasilisha mada ya dalili na madhara ya magonjwa haya Ndugu Flugence Temu ambaye pia ni Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Mpwapwa amesema kuwa: Magonjwa haya kwa ujumla yana madhara makubwa kwa jamii na ametoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hizi. Akieleza dalili za Ugonjwa wa surua ni: homa, mafua na kikohozi kwa mtoto kwa siku chache za mwanzo, macho yanakuwa mekundu na hutoa majimaji, vipele vidogo vidogo hutokea ambavyo huanzia paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima. Pia madhara ya surua ni makubwa kama vile: masikio kutoa usaha ambao huweza kusababisha kutosikia, vidonda vya macho vinavyoweza kusababisha upofu, nimonia, utapiamlo, kuvimba ubongo na kifo.
Aidha Ndug. Temu ameendelea kuzitaja dalili na madhara ya ugonjwa wa rubella; ambazo dalili zake ni: vipele vidogo vidogo, homa, macho kuwa mekundu, uchovu wa mwili, vidonda kooni, uvimbe kwenye matezi na mafua. Madhara ya Rubella ni: matatizo ya moyo, kutosika vizuri, kupata mtoto wa jicho, maambukizi kwenye ubongo na mishipa ya fahamu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amewapongeza wazazi walijitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwaleta watoto wao kupatiwa chanjo na amewasisitizia kuwa watoe taarifa nzuri kwa wenzao wasiofika katika uzinduzi huu wa leo.
Aidha Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi ili kuwapeleka watoto wao ili wapate chanjo hizi. Pia amesisitiza kuwa wote waliohudhuria uzinduzi huu kwa namna moja au nyingine wamejengewa uelewa mkubwa kuhusu chanjo hii na hivyo amewataka kuwa mabalozi wazuri wa kuelezea umuhimu wa chanjo hizi kwa jamii na sio kupotosha.
Kutokana na madhara ya magonjwa haya kuwa makubwa kwa jamii ndio maana, Serikali imeamua kuendesha kampeni cha chanjo kwa nchi nzima. Hivyo nachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali chini ya Wizara ya Afya na maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kwa kuchua hatua madhubuti ili kukabiliana na magonjwa haya hatari.
Vilevile Mhe. Shekimweri ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa kujitokeza kwa wingi katika kujiandiksha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Kauli Mbiu ya kampeni hii ya Chanjo kwa mwaka huu 2019 ni "Chanjo ni kinga kwa pamoja tuwakinge"
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.