Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo tarehe 2 Mei 2019 amegawa Dawa za Minyoo, Matende na Kichocho bure kwa wanafunzi wa shule za msingi Wilayani Mpwapwa. Mkuu wa Wilaya amegawa dawa hizo katika siku ya uzinduzi wa Ugawaji wa Dawa katika Viwanjwa vya Shule ya Msingi Chazungwa.
Katika uzinduzi huo baadhi ya wakuu wa idara na taasisi wamehudhuria, pamoja na Mganga Mkuu wa Wilaya na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Maria Leshalu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amegawa dawa za Kichocho, Matende na Minyoo kwa wanafunzi wa shule za msingi 3 ambazo ni Chazungwa, Mtejeta na Mpwapwa katika uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa dawa za kukinga magonjwa yao. Uzinduzi huo umefanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chazungwa Wilayani Mpwapwa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wataalam wa idara ya Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Katika uzinduzi huo wakuu wa idara, taasisi, wananchi na wanafunzi hususan wa shule za msingi wamehudhuria na kupata elimu iliyotolewa na Daktari Arsen Ngowi juu ya namna ya magonjwa hayo yanavyoweza kuingia kwa binadamu, kuzuia, kujikinga na kutibu. Vile vile Daktari Ngowi amesema "Madhara ya magonjwa haya ni makubwa kama vile kukosa kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kupata vilema vya kutumu, kushambuliwa kwa viungo vya uzazi, tumbo na figo, kupata tatizo la afya ya akili kwa kuathirika kwa ubongo, kuathirika kisaikolojia na kutengwa na jamii". Hivyo Ngowi ametoa wito kwa wazazi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kunywa dawa hizi zinazotolewa bure.
Katika Hotuba yake Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri ameeleza kuwa zoezi la ugawaji wa dawa hizi za minyoo, matende na kichocho ni endelevu katika Wilaya ya Mpwapwa na hivyo ametoa wito kwa wanafunzi pamoja na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika kunywa dawa hizo.
Katika hotuba yake Mhe. Shekimweri amesema "Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kamati ya maandalizi kwa kunikaribisha kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huu muhimu wa unyweshaji wa dawainga/Tiba za magonjwa ya minyoo ya tumbo na Kichocho kwa watoto wetu wa shule za msingi. Aidha niwapongeze wananchi wote wanaozunguka shule zetu za Mtejeta na Chazungwa mlioacha shughuli zenu na kukusanyika nasi kwa ajili ya uzinduzi wa shughuli hii muhimu. Ndugu wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo: IMA WORLD, wamelenga kutoa dawa Kinga/Tiba kwa ajili ya minyoo ya tumbo na kichocho katika Mikoa mbali mbali Tanzania ukiwemo Mkoa wetu wa Dodoma. Serikali imeamua kutoa dawa hizi kwa sababu magonjwa haya hayapewi kipaumbele kama magonjwa mengine (mfano Malaria, HIV na Kifua Kikuu) licha ya kwamba yana madhara makubwa katika jamii na kwa wananchi wetu. Ndugu wananchi, magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele ni pamoja na Ukoma, ugonjwa utokanao na kuumwa na mbwa au mnyama mwenye kichaa (rabies), ugonjwa wa Tauni, Matende na Mabusha au Ngirimaji, Trakoma, Kichocho, Minyoo ya tumbo, Usubi, Homa ya dengi, Homa ya Malale na Homa ya Ini."
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (katikati aliyesimama) akihutubia wananchi katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chazungwa katika Uzinduzi wa Ugawaji na Unywaji Dawa.
Pia Mhe. Shekimweri ameongeza "Ndugu wananchi, magonjwa haya ambayo hayapewi kipaumbele yana madhara makubwa kwa waathirika na kwa Taifa kwa ujumla. Baadhi ya madhara ya magonjwa haya ni maumivu ya muda mrefu na wakati mwingine ulemavu mkubwa, huchangia umaskini na hudumaza uchumi wa taifa, hudhoofisha ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili katika umri mdogo, na vifo kwa waathirika. Bila shaka baadhi yenu mmekutana au kuwaona wagonjwa wenye matende wanavyotaabika na kuumia na pia wale wanaougua kansa ya kibofu cha mkojo au Ini. Hakika madhara haya ni makubwa."
Mkuu wa Wilaya amewasisitiza wananchi kwa kusema "Ndugu wananchi, napenda kuwahakikishia nyinyi nyote kuwa dawa hizi zinazotolewa katika vituo vyetu ni salama na zimethibitishwa na shirika la Afya Duniani (WHO), na zinatolewa na wataalamu wenye uzoefu mkubwa waliobobea katika fani hii kwa muda mrefu. Na asiwepo mtu yeyote kupotosha juu ya zoezi hili. Dawa hizi zinatibu endapo unavyo vimelea vya magonjwa husika na hutukinga na ugonjwa endapo huna vimelea vya ugonjwa". Pia nanyi wanafunzi mkiwa na minyoo au vimelea vya magonjwa kama kichocho afya zenu zitazoofika na uwezo wa kufikiri unapungua na hata hamtaweza kujifunza vizuri na hivyo kushindwa kufikia malengo ya ufauli kishule, Kiwilaya, Kimkoa hadi Kitaifa.
Kutokana na madhara ya magonjwa haya, Serikali yetu ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo IMA WORLD na wengine wanaogharimia mpango huu imeamua kugawa dawa hizi bure bila gharama yoyote kwa wananchi wake ili kuboresha Afya zao.Nisisite kuwa usafi wa mazingira ni nguzo kuu katika kuimarisha Afya zetu. Nawaasa wananchi wote kuhakikisha kuwa mazingira yetu majumbani na sehemu za kazi
yanakuwa safi kila siku. Nanyi wanafunzi mnatakiwa kuwa wasafi, mazingira ya shule zenu siku zote yawe safi. Tumieni vyoo vyenu vizuri ili muepukane na magonjwa ya minyoo na kuhara. Walimu shirikianeni katika zoezi hili la kugawa dawa kwa wanafunzi wenu.
Wanafunzi wa Shule za Msingi Chazungwa, Mtejeta na Mpwapwa wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya na baadae kuanza kunywa dawa
Vilevile Mhe. Shekimweri amesisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuwajali na kuwathamini wananchi wake imeamua kutumia fedha nyingi kwa ajili ya Ununuzi wa dawa hizi ili wananchi wasiweze kuugua magonjwa haya ya minyoo, matende na kichocho. Kwa kuwa Serikali imewathamini, nanyi wananchi mthamini mchango wa Serikali kwa kujitokeza kwa wingi katika kupata dawa na kuzitumia kadri madaktari walivyoeleza.
Kwa maelezo zaidi pakua nyaraka hizi:
HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA MPWAPWA KATIKA UZINDUZI WA UGAWAJI WA DAWA.pdf
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.