(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo amefanya mkutano na Wazee wa Mji wa Mpwapwa ili kuwafahamisha wazee hao miradi inayoendelea katika Wilaya ya Mpwapwa na kusiliza changamoto zao. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa wa Mkuu wa Wilaya na kuhudhuriwa na; Katibu tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Wataalam mbalimbali na wazee.
Wazee hao wana Umoja wao unaoongozwa na Mwenyekiti wao, Mzee Gabriel Mnyawami ambaye amesoma taarifa ya wazee wa Mpwapwa kwa niaba ya wazee wote mbele ya Mkuu wa Wilaya. Katika taarifa hiyo imeeleza chanagmoto na maombi kama yafuatayo:-
1. Huduma ya afya zisizoridhisha kwa wazee na wapatapo huduma, dawa zote huambiwa wakanunue. Pia wameomba zahanati ya Kijiji cha Mbori ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya.
2. Katika kilimo kuwe na zao la biashara.
3. Wameomba waanzishiwe mfuko wa Fedha za Mikopo (Revolving fund) ambapo wanaweza kukopa kwa riba nafuu ili kuweza kuendesha shughuli zao.
4. Wameomba kupata taarifa ya muendelezo wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mpwapwa, barabara ya lami, gari la zima moto na gari la maji taka.
5. Wameomba kuanzishwe Maktaba ya Wilaya, na taarifa ya upugufu wa vyumba vya madarasa na madawati.
6. Wameomba ufafanuzi kwanini Maji hayatoshi na yamekuwa ya shida katika mji wa mpwapwa.
7. Wameomba ufafanuzi kwa nini mradi wa ukumbi wa halmashauri bado ni kiporo.
8. Wameomba Ulinzi na usalama uimarishwe kwa kuwa kuna matapeli wengi katika Mji wa Mpwapwa kwa sasa; mfano eneo la Benki wazee huwa wanatapeliwa.
9. Wamemba ufafanuzi na suluhisho kwa nini TANESCO wanachelewesha kuweka umeme hata baada ya kulipia gharama zote?
Baada ya mada hizo kuwasilishwa, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri ameanza na kufafanua jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayongozwa na Rais Mhe. Dkt. John P. Magufuli katika kuleta maendeleo ya Mpwapwa na Nchi kwa ujumla. Mhe. Shekimweri ameeleza kuwa Serikali inafanya ujenzi wa reli ya treni iendayokasi, barabara zinazounganisha Mikoa na Wilaya, ununuzi wa ndege mpya nane na nyingine mbili zipo hatua ya Ujenzi na kujenga bwawa kubwa la umeme mkoani Morogoro ambapo vyote hivyo vitasaidia katika kukuza uchumi wa Nchi yetu hivyo tuunge mkono jitihada hizo.
Wazee wa Mpwapwa wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa katika kikao kilichofanyika kati ya Wazee hao na Mkuu wa Wilaya (wa pili kusho ni: Mzee Mnyawami Mwenyeikti wa Umoja wa Wazee wa Mpwapwa)
Aidha katika Masuala ya Elimu, Mkuu wa Wilaya ameleeza kuwa; Katika Elimu Serikali imetoa shilingi Milioni miatatu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma katika shule mbalimbali ambayo yamemalizika na yanatumika kwa sasa. Pia katika upanuzi wa Chuo cha Ualimu cha mpwapwa Serikali imetoa shilingi bilioni 2.8 na itajenga Maktaba kubwa ya kisasa ambapo maktaba hiyo itatumika kwa utaratibu utakaopangwa ili kunufaisha watu wote. Vile vile Serikali imejenga Maktaba na Mabwaro ya kisasa katika shule za Sekondari zenye kidato cha tano na sita za Kibakwe, Berege, Mazae na Mpwapwa ili watoto wetu waendelee kupata elimu bora.
Pia katika Afya Mhe. Shekimweri amesema kuwa; Kwa ujumla huduma za afya zimeimarika, changamoto zilizopo ni za kibinadamu kama kufanya kazi kwa mazoea na maadili mabovu hivyo wazee wangu tusaidiane kuwaongoza vijana wetu kuwa waadilifu, kuwajengea uwezo na kuwakemea na wasipojirekebisha watachukuliwa hatua. Kupitia fursa hii namuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kuwa Orodha ya dawa kwa ngazi zote zibandikwe ili watu waweze kuona ni dawa zipi zinapatikana. Pia, tumepoke shilingi bilioni 1 na milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya Mima, Kibakwe na Pwaga. Hata hivyo katika kipindi hiki cha miaka minne tumepokea gari la wagonjwa (ambulance) mpya ya kituo cha Rudi, pia tumepewa shilingi Milioni 96 kwa ajili ya kukamilisha vituo vya afya. Vilevile Wilaya yetu ina changamoto ya Utapiamlo mkali ambapo tumejengewa jengo kwa ajili ya huduma za kuaanda lishe bora.
Pia Mkuu wa Wilaya ameeleza masuala ya kilimo kuwa; nawaomba wazee wangu tuendelee kuhimizana kulima kwa juhudi na kuondoka kabisa na dhana ya chakula cha msaada kwa kuwa hakipo kabisa, msimu wa kilimo hakuna watu kucheza pool table wafanye kazi na kulima mazao ya chakula na biashara kama korosho ili kuinua kipato cha familia na Halmashauri. ..
Wazee wa Mpwapwa wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa katika kikao kilichofanyika kati ya Wazee hao na Mkuu wa Wilaya
Akiendelea kueleza Mkuu wa Wilaya amesema kuwa; katika wilaya ya Mpwapwa kuna barabara yenye urefu wa KM 1023 ambayo ipo chini ya TARURA na barabara yenye urefu wa KM 316 inasimamiwa na TANROADS. Katika miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano kuna barabara nyingi zimejengwa kama Kidenge - Lufu ambayo tangu tupate uhuru hawajawahi kuwa na barabara ya Kizi - Mbuga hadi Lumuma. Pia kuna barabara ya lami katika eneo la Mpwapwa Mjini yenye urefu wa KM 2.5 ambapo ujenzi unaendelea na ujenzi huo wa barabara za lami hapa mjini utazingatia pia uwekaji wa taa barabarani.
Aidha, katika masuala ya upatikanaji wa maji Mkuu wa Wilaya amekiri kuwa; Ni kweli mji wa Mpwapwa una uhaba wa maji, na katika ujio wa waziri wa maji Mpwapwa tulimueleza kuwa tunahitaji chanzo kipya cha maji. Pia serikali ilitoa shilingi bilioni 4.7 kwa miradi 10 ya maji ambayo ipo 90% ya umaliziaji na pindi itakapo kamilika uhaba wa maji kwa wilaya ya Mpwapwa utapungua.
Mkuu wa Wilaya pia amezungumzia masuala ya umeme, ambapo ameeleza kuwa; kwa maelezo ya waziri wa nishati kuwa mbunge wa Kibake Mhe. George Simbachawene alitusaidia sana kuviingiza vijiji vyote vya Mpwapwa katika mpango wa kuwekewa umeme. Hadi kufikia 2021 vijiji vyote vya Mpwapwa na vitongoji vyake vitakuwa na umeme wa mradi wa REA unaoendelea. Hata hivyo amewahakikishia wazee kuwa wananchi wote ambao wamecheleweshwa kuunganishiwa umeme baada ya kulipia wawasilishe orodha ya majina yao na mahali wanapoishi ili afanye mawasiliano na meneja wa TANESCO ili waweze kupata huduma hiyo.
Wazee wa Mpwapwa wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa majibu mazuri ya kutatua changamoto zao na ufafanuzi mzuri alioutoa katika kikao hicho. Pia wamemuomba Mkuu wa Wilaya kuwa asichoke kuwasikiliza maana wazee wanachangamoto nyingi na wa kuzitatua ni yeye.
Akifunga kikao hicho Mkuu wa Wilaya amewashukuru wazee kwa umoja wao na kukusanyika hapo ili kusikiliza mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano. Pia amewapongeza wazee kwa kuwasilisha changamoto zenye tija kwa Wilaya yetu na ameahidi kuzitatua kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa miradi husika kama maji, barabara, afya, kilimo, elimu na umeme.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.