Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amekagua Ujenzi wa Barabara ya Lami Mpwapwa Mjini ambayo yenye takribani jumla ya KM 2 na yenye thamani ya Tsh 900,000,000/= kwa vipande vya kutoka Round about kwenda Polisi na kutoka Kizota Filling station kwenda 4 ways, 4ways kwenda Halmashauri na Magomeni kwenda Duka la Mmasi.
Barabara hiyo inajengwa na Wakandalasi wawili, Mkandalasi mmoja toka Kampuni ya GS Contractors (T) LTD ya Iringa, anajenga barabara ya kutoka Kizota Filling station kwenda 4 Ways, kipande cha kutoka Halmashauri kwenda 4 Ways na Magomeni kwenda Duka la Mmasi. Mpaka sasa ujenzi wa barabara ya yenye urefu wa KM 1.12 na upanda wa mita 6 umefikia 20% ambapo barabara yote itagharimu kiasi cha Tsh 441,630,000/= hadi itakapokamilika. Ujenzi huo utatumia muda wa miezi 6 kulingana na mkataba.
Aidha Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandishi Emmanuel Lukumay ameeleza kuwa "Kipande cha kutoka Round about hadi Polisi chenye takribani Meta 800 kitajengwa na Mkandalasi mwingine ambaye ataanza kazi wiki ijayo na vifaa vyake ameshavileta".
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wapili kulia) akipata maelezo ya ujenzi wa barabara ya Mpwapwa Mjini katika kipande cha kutoka Kizota Filling Station hadi 4 Ways.
Mkuu wa Wilaya amepata maelezo ya kina juu ya ujenzi wa barabara hii na amewakumbusha Mkandalasi wa Kampuni ya GS Contractor (T) LTD Mhandisi Omari Ally na Mhandisi Emmanuel Lukumay ambaye ni Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuwa wawe wanafanya Mkutano katika sehemu ya kazi (site meeting) na kufanya majaribio ya kila hatua kama miongozo ya uhandisi unavyohitaji. Pia Mkuu wa Wilaya amehoji kama kutakuwa na taa za barabarani, mkandalasi amejibu kuwa hakutakuwa na taa za barabarani kwa kuwa bajeti hairuhusu. Kufuatia jibu la Mkandalasi Mkuu wa Wilaya ametoa ushauri kuwa wanaweza kuweka alama za kuweka taa za barabarani kwa ajili ya hapo baadae maana hapo baadae tusije tukaharibu barabara kwa kuweka taa za barabarani.
Aidha Mhe. Shekimweri amekuwashukuru wananchi wa kata ya Mpwapwa Mjini kwa kuamua kubomoa vibanda na baraza za maduka yao ili kupisha ujenzi wa barabara ya lami Mpwapwa Mjini. Pia amewapongeza wafanyakazi wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maji na Simu (TTCL) kwa kuwaweza kuhamisha miundombinu yao bila kuathiri huduma kwa wananchi ili kupisha mradi huu wa barabara ya Lami.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (kulia) akipata maelezo toka kwa Meneja wa TARURA juu ya ujenzi wa barabara ya lami Mpwapwa Mjini katika kipande cha kutoka 4 ways hadi Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Aidha Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Emmanuel Lukumay amesema "barabara hii itachukua muda wa miezi sita kumamilika kama mkataba unavyosema, hivyo mradi huu utasaidia kuboresha mji wa Mpwapwa ambao ni mji mkongwe na kuondokana na kuwa na barabara za changarawe ambazo huharibika mara kwa mara". Pia Meneja wa TARURA ameongeza kuwa "sisi kama TARURA tumejipanga vizuri na tumeshapima udongo katika barabara yenye urefu wa KM 2 na kusanifu, na mwaka huu tutasanifu (design) tena km 4". Vilevile Meneja wa TARURA ametoa wito kwa mkatandalasi afanye kazi kizalendo bila kusimamiwa na mtu yoyote kwa kuwa mradi huu utakaguliwa na viongozi mbalimbali.
Pia diwani wa kata ya Mpwapwa Mjini Mhe. George Fuime amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha ya kujenga barabara ya lami Mpwapwa Mjini. Pia amewashukuru wananchi wa Kata ya Mpwapwa Mjini kuweza kubomoa miundombinu yao mbalimbali kwa ajili ya kupisha mradi huu wa barabara ya lami na kutoa wito wa kutunza miundombinu ya barabara hii.
Mhe. Shekimweri amemtaka mkandalasi kumaliza kazi za kuweka vifusi na kushindilia barabara mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza maana mvua za Mpwapwa hunyesha kwa muda mfupi ila athari yake ni kubwa, hivyo inaweza kusababisha vifusi vyote kusombwa na maji.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.