(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amefungua Kikao cha maandalizi ya Kampeni ya Chanjo ya Magonjwa hatari ya Surua, Rubella na Polio. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Wilaya na kuhudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime, baadhi ya waheshimiwa madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Paul Sweya, Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wakuu wa idara na wataalam wa Afya akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari. Archard Rwezaula.
Akiwasilisha taarifa katika kikao hicho Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Daktari. Rwezaula amesema " Wilaya ya Mpwapwa ni miongoni mwa wilaya zinazoshiriki zoezi la uendeshaji wa kampeni ya chanjo ya kitaifa za Surua, Rubella na Polio ya sindano kwa watoto chini ya miaka mitano (5)" . Pia ameongeza kuwa "Watoto wanaolengwa katika zoezi hili ni wale walio na umri kati ya miezi 9 hadi miezi 59 hawa watapatiwa chanjo ya Surua na idadi yao wapata watoto 55,603 na watoto wanaostahili kupata chanjo ya Polio ya sindano ni wenye umri kati ya miezi 18 hadi 42 (yaani mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu na nusu) ambao wapo 26,538".
Wajumbe waliohudhuria kikao cha Kampeni ya Chanjo ya Surua, Rubella na Polio ya sindano wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya
Chanjo hii itaanza tarehe 17/10/2019 hadi tarehe 21/10/2019 ambapo itachukua muda wa siku tano katika utekelezaji wake; na maeneo yatakayohusika na utoaji wa chanjo ni vituo vya kudumu ambavyo ni zahanati, Vituo vya afya, Hospitali na Vituo vya Kuhamahama hasa sehemu ambazo hakuna zahanati inaweza kutolewa kwenye ofisi za shule, kijiji, sokoni au Godown kadri ya mazingira yatavyoruhusu ili kuhakikisha kila mlengwa amefikiwa.
Akiwasilisha mada ya dalili na madhara ya magonjwa haya Ndugu Flugence Temu ambaye pia ni Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Mpwapwa amesema kuwa: Magonjwa haya kwa ujumla yana madhara makubwa kwa jamii na ametoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hizi. Akitolea mfano wa dalili za Ugonjwa wa surua ni: homa, mafua na kikohozi kwa mtoto kwa siku chache za mwanzo, macho yanakuwa mekundu na hutoa majimaji, vipele vidogo vidogo hutokea ambavyo huanzia paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima. Pia madhara ya surua ni makubwa kama vile: masikio kutoa usaha ambao huweza kusababisha kutosikia, vidonda vya macho vinavyoweza kusababisha upofu, nimonia, utapiamlo, kuvimba ubongo na kifo.
Aidha Ndug. Temu ameendelea kuzitaja dalili na madhara ya ugonjwa wa rubella; ambazo dalili zake ni: vipele vidogo vidogo, homa, macho kuwa mekundu, uchvu wa mwili, vidonda kooni, uvimbe kwenye matezi na mafua. Madhara ya Rubella ni: matatizo ya moyo, kutosika vizuri, kupata mtoto wa jicho, maambukizi kwenye ubongo na mishipa ya fahamu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amepongeza utangulizi wa Mganga Mkuu wa Wilaya kuwa amegusa nyanja zote muhimu katika shughuli nzima, pia amempongeza Ndugu. Temu kwa kuwasilisha mada vizuri na kuanisha madhara yatakayopatikana kama watoto wasipopata chanjo hizi.
Aidha Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi ili kuwapeleka watoto wao ili wapate chanjo hizi. Pia amesisitiza kuwa wajumbe waliopatiwa mafunzo au kujengewa uelewa wanatakiwa kuwa mabalozi wazuri wa kuelezea umuhimu wa chanjo hizi kwa jamii na sio kupotosha.
Kauli Mbiu ya kampeni hii ya Chanjo kwa mwaka huu 2019 ni "Chanjo ni kinga kwa pamoja tuwakinge"
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.