(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa).
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul Mamba Sweya ameweka utaratibu wa Wakuu wa idara na Vitengo vya Halmashauri hiyo kutembelea na kukagua ujenzi wa Miradi ya maendeleo. Ndugu. Sweya amefikia uamuzi huo baada ya miradi mingi kutoendana na kasi anayoihitaji pamoja kutokufika muda uliowekwa katika mkataba wa ujenzi wa miradi hiyo. Akiwa katika kikao cha Wakuu wa Idara Mkurugenzi amesema kuanzia sasa timu ya wakuu wa idara itakuwa inaambatana nae ili kwenda vijijini kuhamasisha kasi ya ujenzi wa miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa ikiwepo Madarasa, mabwalo ya chakula, maktaba, vituo vya afya, mifereji ya kilimo cha umwagiliaji na vyoo.
Wakuu wa idara kwa pamoja wamepongeza wazo hilo la mkurugenzi na kuanzia leo wameanza safari ya kutembelea ujenzi wa Maktaba, Madarasa na Bwalo katika Shule ya sekondari Kibakwe.
Mkurugenzi mtendaji pamoja na Wakuu wa idara wametembelea miradi ifuatayo:-
Shule ya Sekondari Kibakwe.
Shule hii imepata fedha toka serikali Kuu kiasi cha Tsh. 175,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa Bwalo, Maktaba na Madarasa matatu ambapo kwa sasa mawili yamekabilika bado darasa moja ambalo lipo katika hatua ya madirisha, bwalo lipo katika hatua ya kumwaga jamvi na maktaba ipo katika hatua ukamilishaji wa boma. Aidha wakuu wa idara wamefanya kikao cha ndani pamoja na kamati ya ujenzi, uongozi wa shule na mratibu wa Elimu Kata ya Kibakwe ili kujua kwa nini wamechelewa kumaliaza mapema kwa kuwa muda wa mwisho kumaliza ulikuwa ni tarehe 22 Aprili 2019.
Afisa Mtendaji wa kata ya Kibakwe Ndugu Baraka Zebedayo amewaeleza wakuu wa idara kuwa Kilichosababisha ujenzi kusuasua ni mwamko hafifu wa wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo, ila baada ya kuweka mikakati dhatibi viongozi wa vijiji na kata wamekusanya fedha na kwa sasa ujenzi unaendelea vizuri na tutamaliza kabla ya mwezi Juni kuisha. Ndugu. Zebedayo amesema kuwa kwa sasa kila kitu kipo katika site na ujenzi uko vizuri.
Mkurugenzi amemuagiza Mkuu wa Shule wa Kibakwe kushirikiana na mafundi katika kuandaa mpango kazi ili kujua kama tuko nyuma au tunaenda sawa na mpangokazi wetu. Pia ameagiza mikataba yote ya ujenzi wa majengo haya irejewe upya kwa kuleta Halmashauri ili mwanasheria aweze kuipitia na kushauri kisheria.
Katika kikao hicho Afisa Utumishi wa Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Pius Sayayi ametumia fursa hii kuwaelimisha kamati ya ujenzi, uongozi wa shule na viongozi wa kata na vijiji kuwaelimisha juu ya maana ya Force Account ambapo kamati za ujenzi ndio zinakuwa wasimamizi wa miradi husika kwa kujengewa uwezo na wataalam wa Halmashauri akiwemo Afisa Manunuzi, Mhandishi wa Wilaya, Mwanasheria wa Wilaya. Pia ameeleza kuwa watumishi wanaongozwa na sheria za utumishi wa umma na hivyo amewaasa kusimamia fedha hizo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Ujenzi unaendelea kwa kasi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Kibakwe likiwa katika hatua ya kuweka nguzo na jamvi.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Kibakwe.
Katika kutembelea Kituo cha Afya Kibakwe kilichopewa Tsh 500,000,000/= kilichofikia hatua za umaliziaji ikwemo kuweka jipsam katika vyumba vitatu katika jengo la Mapokezi, kuweka vigae katika vyoo, kufunga umeme, ili kumalizia. Hali hii imesababishwa na fundi kutokuwa na kasi ya kuridhisha ili kumaliza kazi hii, kufuatia hali hii Mkurugenzi amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu kutoa Tsh. 1,300,000/= kwa ajili ya umaliziaji wa kununua mbao, vigae, skatingi, masinki ya vyoo na jipsam. Kwa kuwa fundi huyo anasuasua kumaliza kazi Mkurugenzi Amemuagiza Mtendaji wa kata aite viongozi na kamati ili kuondoa fundi hiyo mara moja.
"Hatuwezi kumbembeleza fundi huyo kwa muda wa miezi saba mpaka sasa, aondolewe mara moja maana hakuna changamoto inayomsababisha asifanyekazi" amesema Ndugu. Sweya. Baada ya ukaguzi wa majengo Wakuu wa Idara wamepata fursa ya kwenda stoo kukagua vifaa vilivyobaki ili kijiridhiisha kama vifaa vilivyopo vitatosha kumalizisha sehemu iliyobaki, baada ya kukagua stoo imeonekana kuwa na vifaa vyote na vitatosha.
Wakuu wa idara wakikagua majengo ya kituo cha Afya kibakwe yakiwa katika hatua za mwisho kukamilishwa.
Shule ya Sekondari Berege.
Katika shule hii kuna ujenzi wa bwalo, maktaba na madarasa ambapo kwa upande wa madarasa mawili yamekamilika katika hatua ya boma na wanapiga lipu, maktaba ipo katika hatua ya lenta, na bwalo lipo katika hatua ya jamvi. Pia Makamu Mkuu wa Shule amewahakikishia wakuu wa idara kuwa kwa sasa vifaa vyote vipo na ujenzi utaenda haraka. Kufuatia kauli hiyo ya Makamu Mkuu wa Shule; Mkurugenzi ameagiza kuwepo na mpango kazi wa shughuli zote za ujenzi na mwisho wa kukamilisha majengo yote ni tarehe 15 Juni 2019. Pia Wakuu wa Idara wamepongeza kazi na kasi ya ujenzi inavyoenda.
Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Mpwapwa Ndu. Paul Sweya (kulia) akitoa mfano wa namna sahihi ya kumwagia maji matofali yaliyopo pendeni mwa jengo la bwalo linaloendea kujengwa ambapo lipo katika hatua ya kuweka jamvi na kusuka nondo kwa ajili ya nguzo katika hule ya Sekondari Berege.
Shule ya Sekondari Mazae.
Katika Shule hii kuna ujenzi wa bwalo ambalo lipo katika hatua ya madirisha, kujenga kuta na nguzo; maktaba imefikia hatua ya visusi na kwa sasa imekamilika imebaki kuezeka na changamoto ni kuwa mbao na bati bado hazijanunuliwa mpaka sasa. Mkurugenzi ameagiza kuwa Afisa Manunuzi wa Shule hiyo Bwana Modekai aende katika Kiwanda cha Sao Hill kununua mbao kwa ajili ya kuanza kupaua mara moja. Pia ameagiza bati za kuezekea pia zinunuliwe mapema kwa mkupuo ili bei yake ipungue na zinunuliwe kiwandani ili kununua kwa bei nafuu. Vile vile ameagiza kuwa Mpangokazi uandaliwe mara moja na mikataba yote iletwe Halmashauri kwa mwanasheria kwa ajiri ya kurejewa.
Ujenzi unaendelea kwa kasi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Mazae likiwa katika hatua ya kuweka nguzo na kuta.
Shule ya Sekondari Chunyu.
Katika shule hii kunajengwa madarasa mawili ambayo yapo katika hatua ya msingi na ila ujenzi unaridhisha kwa kasi yake. Mtendaji wa Kata Bwana Hemedi amewaeleza wakuu wa idara kuwa kwa sasa vifaa vyote vipo mfano; matofali, mchanga, kifusi, mawe na kokoto hivyo ujenzi utaenda kasi na kumaliza kwa wakati. Wakuu wa idara wamepongeza hatua iliyofikiwa na wametoa ushauri kuwa waongeze kasi na usimamizi wa karibu ili kumaliza kwa wakati kabla ya tarehe 25 Juni 2019.
Ujenzi unaendelea kwa kasi wa boma la madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Chunyu likiwa katika hatua ya Msingi.
Wananchi na viongozi wa kata na vijiji kwa pamoja wamefurahi sana kutembelea na wakuu wa idara na kuwahamasisha kusimamia miradi hii, hivyo wameomba zoezi hili liendelee hasa kwa maeneo ambayo miradi inasuasua.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.