(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri leo amefunga rasmi mafunzo ya mgambo yaliyofanyika katika kata ya Chitemo Wilayani Mpwapwa. Katika kufunga mafunzo hayo Mhe. Shekimweri amekagua maonesho mbalimbali ya mbinu za kivita walizooneshwa na wanamgambo hao mahili. Wanamgambo hao wameonesha mbinu ikiwemo za kujificha katika maandaki, kupita katika vizingiti, kupita katika kifaru cha kamba na kupita juu ya kamba kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Mmoja wa wanamgambo waliopata mafunzo akipita juu ya kamba iliyofungwa katika miti miwili mirefu katika Kata ya Chitemo
Mkuu wa Wilaya amewapongeza sana wanamgambo hao kwa kuhitimu mafunzo yao wakiwa wameiva vizuri na kuwa wakakavu. Pia ametoa wito kwa wananchi wote kuwaruhusu vijana wao kujiunga na mafunzo ya mgambo kwa kuwa mgambo wanasaidia sana katika ulinzi na usalama katika ngazi ya kata na kijiji.
Ameupongeza uongozi wa kata ya Chitemo kwa kukubali mafunzo haya kufanyika katika kata hii na kuweza kuyagharimia, hii ni kwa kuwa mafunzo haya yana umuhimu mkubwa sana hasa katika ulinzi na usalama wa kata hii na kata za jirani.
Mkuuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wa kwanza mbele) akienda kukagua maonesho ya wanamgambo waliopata mafunzo
Aidha Mhe. Shekimweri ametoa zawadi ya pesa taslim Tsh. 10,000/= kwa mwanamgambo mmoja aliyepita kwenye kizingiti kwa umahili mkubwa bila kutetemeka.
Pia wanamgambo wametengeneza mradi wao wa ufugaji wa samaki kama Mradi wa Kikundi cha wanamgombo wa Chitemo ambapo wamechimba shimo la kufugia samaki na sasa wanasubiri mvua tu ili waweze kupata maji na kuanza kazi ya kufuga samaki.
Mkuuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wa nne kushoto) akishuhudia maonesho ya wanamgambo waliopata mafunzo
Kwa upande wake Mhe. Shekimweri amewapongeza wanamgambo hao kwa kuanzisha mradi huo na amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul M. Sweya kukiwezesha kikundi hiki cha Mgambo kwa kuwapatia wataalam washauri wa ufugaji wa samaki na fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli hii ya kiuchumi.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.