Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Hemed Suleiman Abdulla amewaongoza viongozi wa serikali, chama, wanafamilia, waislamu na wananchi wa Zanzibar kwenye dua maalum (hitma) ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume
Alhaj Hemed aliongoza hafla hiyo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi, hafla iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuzuru kaburi la hayati mzee Karume ambapo viongozi wa madhehebu mbalimbali walipata fursa ya kumuombea dua kiongozi huyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Khamis Juma amesema ni jambo jema na la faraja kuwakumbuka na kuwaombea dua viongozi waliotangulia mbele ya haki ambao walijitoa katika kulipigania Taifa.
Sheikh Khamis amewataka wananchi kuendeleza umoja, amani na mshikamano mambo ambavyo vilisimamiwa na viongozi waasisi wa Zanzibar na ndio chachu ya maendeleo yaliyofikiwa hapa nchini.
Akimzungumzia hayati Mzee Karume, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Masato Wasira amesema kiongozi huyo alijitoa katika kuwapigania wazanzibari kuondokana na dhuluma pamoja na kusimamia haki, usawa na uzalendo katika kulijenga Taifa na ndio sababu kubwa ya kufanyika kwa mapinduzi Matukufuya mwaka 1964.
Wasira amesema suala la elimu na matibu bure lilipewa kipaombele na Mzee karume ikiwa ni falsafa yake ya kupingana na adui ujinga, maradhi na njaa jambo ambalo linaendelezwa na viongozi waliopo sasa madarakani.
Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ndugu Khamis Abdalla Said amesema Marehemu Mzee Karume ameacha alama katika sekta ya elimu ambapo maendeleo makubwa ya elimu yaliyopo sasa yanatokana na misingi imara iliyoekwa na kiongozi huyo.
Alisema lengo la Mzee Karume kutangaza elimu bure lilikuwani kuhakikisha watoto wa wakwezi na wakulima wanapata elimu bila ya malipo ili kujenga Taifa imara la baadae jambo linaloendelea kuenziwa na viongozi waliopo madarakani.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.