Na: Shaibu J. Masasi; Afisa TEHAMA - Mpwapwa Dc.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sarah J. Komba amemuita Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Viettel Tanzania/Halotel tawi la Dodoma Ndugu. Tran The Hoang katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa. Kikao hicho kimehudhuriwa na Wananchi wa Kijiji cha Berege ambapo Mnara Umejengwa katika kijiji hicho na Kampuni ya Halotel ila hailipi mapato ya kijiji, Watu binafsi akiwemo Mzee Mzee Sepetu ambaye Mnara wa Halotel umejengwa kwenye eneo lake lakini halipwi fedha, watendaji wa vijiji na kata za Berege na Matomondo.
Aidha kikao hicho kimedhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Paul M. Sweya pamoja na Wataalam toka Halmashauri ya Wiaya ya Mpwapwa akiwemo Afisa Ardhi, Mwanasheria na Afisa TEHAMA.
Katibu Tawala amefikia uamuzi huo kwa kuwa kampuni ya Halotel imekuwa ikilalamikiwa na watu binafsi na taasisi kuhusu mikataba yao ina vipengele vinavyombana mwananchi, kiasi cha fedha kinacholipwa kwa malipo ya kupangisha eneo lilijengwa mnara ni kidogo, wanapobomoa au kujenga mnara huwa hawafuati utaratibu wa kupata kibali, kutolipa malipo ya minara kwa wakati, pia migogoro ya ardhi iliyosababishwa na kujenga minara katika maeneo yasiyo sahihi au kuingia mkataba na kumlipa fedha mtu asiyekuwa mmiliki wa eneo.
Baada ya Majadiliano, Wawakilishi wa Kampuni ya Halotel akiwemo Mkurugeni wa Halotel tawi la Dodoma wameshindwa kutoa majibu ya kuridhisha na kujitosheleza kwa wajumbe waliohudhiria kikao hicho kwa hoja zilizowasilishwa.
Wawakilishi wa taasisi na watu binafsi wenye madai mbalimbali kwa kampuni ya Halotel wakiwa na wawakilishi wa Kampuni ya Halotel katika kikao cha pamoja kilichoitishwa na Mhe. Sarah Komba (wa pili kushoto waliokaa meza kuu) Katibu Tawala Wilaya ya Mpwapwa
Baada ya Wawakilishi wa Kampuni ya Halotel kushindwa kujibu hoja zilizowasilishwa, Katibu Tawala ameiagiza kampuni ya Halotel baada ya Mwezi Mmoja katika kikao kijacho cha tarehe 20 Aprili 2020 walete majibu:- majibu yajikite katika Vipengele vya mikataba vikarekebishwe, mikataba katika minara yote ionekane na ijulikane kwa wamiliki halisi, kuongeza viwango vya kodi/malipo kadri ilivyopendekezwa, kulipa kwa wakati malipo ya pango la minara, na kuleta nyaraka za ushahidi kuwa Mzee Sepetu alikuwa analipwa fedha za mnara kwa miezi ya nyuma. Pia ameongeza kuwa "katika kikao kijacho cha tarehe 20 Aprili 2020 nahitaji kumuona Mkurugenzi Mkuu wa Halotel anayeshughulikia mikataba yote ya minara Tanzania na awe na majibu ya hoja zote zilizotolewa ".
Hata hivyo Mhe. Sarah Komba ameipongeza Kampuni ya Halotel kwa kujenga minara 20 na kufanikisha mawasiliano ya mtandao huo maeneo yote ya Wilaya ya Mpwapwa. Pia ameongeza kuwa asilimia 90 ya wanatumia simu za mkono katika Wilaya ya Mpwapwa wanatumia laini za Halotel, hivyo kampuni hii inafanya vizuri katika sekta ya mawasiliano kwenye Wilaya yetu.
***Mwisho***
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.