Na: Khamlo Njovu - Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mpwapwa
Kamati ya Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya Wilaya ya Mpwapwa imepatiwa mafunzo ya kuijengea uwezo juu ya Sheria namba 9 ya mwaka 2010 ya Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu. Chama cha Watu Wasioona cha Tanzania Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wao wa Utetezi kwa Watu Wenye Ulemavu wamesaidia kuendesha mafunzo haya kwa Kamati wakiwashirikisha viongozi wa vyama vya Watu Wenye Ulemavu wa ngozi, viungo, wasioona na wasiosikia kwa muda wa siku mbili yaani kuanzia tarehe 31/8/2018 hadi 1/9/2018.
Mwezeshaji wa mafunzo toka Chama cha Watu Wenye Ulemavu Taifa, Ndug. Novath Rukwago ambaye ni Mwanasheria wa chama hicho akitoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu pamoja na wadau wengine waliohudhuria mafunzo hayo
Kabla ya kuanza mafunzo wajumbe wakimchagua Bi. Magadalena Mazembe Mazemba kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati kwa kupata kura nne kati ya kura saba zilizopigwa akimshinda Bi. Grace Mhechela aliyepata kura tatu. Mwenyekiti wa Kamati hii ni Mhe. George Malima Lubeleje ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa.
Baada ya shughuli za uchaguzi kukamilika, Mgeni rasmi Ndug. Paul Mamba Sweya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa alifungua rasmi mafunzo haya kwa kueleza kuwa;-
Kamati hii ina majukumu mengi na makubwa katika kuboresha ustawi na maendeleo ya watu wenye ulemavu, hivyo pamoja na majukumu mengi tuliyonayo niwaombe mtumie muda wetu mwingi kuhakikisha ndugu zetu hawa wanapata huduma stahili kama wale wasio na ulemavu wanazipata.Tukumbuke kuwa sisi sote ni walemavu watarajiwa kwani wale wenye ulemavu hawakuumbwa wawe walemavu. Najua kwenye mafunzo haya tutapata muda wa kujua mengi juu ya Sheria inayohudumia watu wenye ulemavu pia majukumu ya Kamati, kwa kifupi Kamati yetu inamajukumu yafuatayo:
i.Kutekeleza maelekezo mbalimbali kuhusiana na watu wenye ulemavu katika wilaya
ii.Kuratibu shughuli zote za watu wenye ulemavu katika wilaya
iii.Kulinda na kuendeleza masuala yote yanayohusiana na ustawi na maendeleo ya watu wenye ulemavu katika wilaya
iv.Kupokea taarifa za utekelezaji za vipindi mbalimbali toka kwenye Kamati za Vijiji au Mitaa
v.Kuwasilisha taarifa za kina za robo mwaka kwa Kamati ya Watu Wenye Ulemavu Mkoa
vi.Kupokea na kuamua malalamiko kuhusiana na Watu Wenye Ulemavu
vii.Kutunza kumbukumbu sahihi za vikao vya Kamati
viii.Kutunza takwimu au rejesta ya watu wenye ulemavu kwenye eneo la Halmashauri.
Hivyo mtaona tulivyo na kazi kubwa ya kuwahudumia watu wenye Ulemavu ikizingatiwa kuwa majukumu haya ni ya kujitolea hivyo tunatakiwa kujizatiti sana ili malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa Watu wenye Ulemavu yaweze kutimia.
Ndug. Khamlo Njovu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mpwapwa akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya Watu Wenye Ulemavu katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa
Mafunzo haya yatatusaidia kuifahamu vyema Sheria ya Watu wenye ulemavu ambayo toka ilipoanzishwa mwaka 2010 kwanza ilikuwa haifahamiki kwa jamii, kwa watekelezaji na hata kwa Watu wenye ulemavu wenyewe. Serikali kwa upande wake itaendelea kuisimamia Sheria hii kwa kuondoa na kutimiza mahitaji stahili ya Watu wenye ulemavu, miundo mbinu inayojengwa kama vile shule, zahanati, Vituo vya Afya, majengo ya biashara, masoko na utoaji wa mikopo kwa ajili ya wanawake na vijana walemavu yanapatiwa kipaumbele ambapo Halmashauri ya Wilaya Katika bajeti yake kwa mwaka 2018/19 imetenga asilimia 2 kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu. Pia tutahakikisha Kamati za Huduma kwa Watu wenye ulemavu na Mahitaji Maalum kwenye ngazi zote za utawala za vijiji na Kata zinaundwa baada ya Kamati ya Wilaya kuanza kazi. Wilaya itaweka utaratibu wa namna ya kutekeleza shughuli za Watu Wenye Ulemavu kwa ngazi zilizotajwa ili kuwezesha upatikanaji wa haki na fursa sawa kwa watu hao.
Halmashauri ya Wilaya itaboresha daftari la Watu Wenye Ulemavu na Wenye mahitaji Maalum ili kuwa na kumbukumbu sahihi za walemavu wote.
Baaba ya mafunzo wajumbe wameazimia kuhakikisha taarifa za Watu Wenye Ulemavu zinapatikana ifikapo Septemba 30, 2018. Pia kamati za huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ngazi ya Kata na Vijiji zinzundwa au kuanzishwa na tathimini ya hali ya miundombinu iliyopo katika ofisi za serikali na mahali pa kutolea huduma katika Wilaya nzima ya Mpwapwa kama ni rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu inafanyika ifikapo Oktoba 2018.
Kwa taarifa zaidi pakua nyaraka hii hapa chini:
HOTUBA YA MGENI RASMI -SIKU YA HUDUMA KWA WATU WENYE ULEMAVU.pdf
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.