Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 826KJ kilichopo wilaya ya Mpwapwa wamebuni mbinu mpya ya unjenzi wa majengo kwa kutumia matofali yalichanganywa kwa udongo na saruji kidogo yenye gharama nafuu. Matofali haya hutengenezwa kwa mashine maalamu huitwa Hydro Form Machine inayotumia mafuta ya diesel au umemem kutegemeana na aina ya injini.
Kambi hiyo ya jeshi imeanzisha ujenzi wa zahanati kubwa yenye wodi 4 (watoto, wanawake, wazazi na wanaume), chumba cha upasuaji 1, vyumba vya madaktari 3, vyumba 2 vya Watu Mashuhuri (VIP), maabara 1 na chumba cha mikutano ya madaktari na wauguzi. Pia kila chumba au wodi ina vyoo vya ndani kwa jinsia zote mbili yaani Ke na Me.
Kufuatia kikosi hicho cha jeshi la JKT kujenga jengo la zahanati kubwa kwa gharama nafuu ambalo litagharimu kiasi cha Tsh.200,000,000/-mpaka kuisha ambapo kwa matofali ya block ingekuwa ni zaidi ya Tsh.500,000,000/=, ndipo Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amewaomba wajumbe wa Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango, Kamati ya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara wa Halmashauri wilaya ya Mpwapwa kwenda kambini hapo kwa lengo ya kujifunza teknolojia hiyo yenye gharama nafuu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wa pili kutoka kushoto) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Donalth Nghwenzi (wa tatu kutoka kushoto) pamoja na wajumbe wengine wa kamati ya FedhaUongozi na Mipango, kamati ya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara wakichunguza matofali yaliyotengenezwa kwa kutumia Mashine ya Hydro Form. (Picha Na. Shaibu J. Masasi - Afisa TEHAMA , Mpwapwa)
Aidha kamanda wa JKT ambaye ndiye mwenyeji wa kuongoza msafara wa wageni toka wilaya ya Mpwapwa akieleza kuhusu ujenzi huo ulivyo nafuu amesema "Matofali ya kutengenezwa kwa mashine ya hydro form ni nafuu sana ukilinganisha na yale ya kutumia tofali za block, kwa kuwa matofali haya yanatumia udogo wa kawaidai, maji kidogo na saruji kidogo. Pia ameleza, katika mfumo mmoja wa saruji wanatengeneza matofauli 150 ya inchi 5 na matofali 70 ya inchi 9 ambapo kwa tofali za block utahitaji mchanga mwingi na saruji nyingi". Vilevile ameeleza kuwa ujenzi wa matofali haya hupangwa tu bila kuweka saruji ila saruji inatumika kwa kuweka plasta kwa upande wa ndani tu, upande wa nje wa jengo na nje wanaweka rangi nzito (water proof) kwa ajili ya kuziba nafasi kati ya tofali na tofali pamoja na kuzuia maji kumomonyoa tofali.
Jengo la Zahanati ya JKT linalojengwa kwa Matofali yaliyotengenezwa kwa mashine ya Hydro Form (Picha Na. Shaibu J. Masasi - Afisa TEHAMA , Mpwapwa)
Waheshimiwa madiwani ambao ni wajumbe wa kamati ya Fedha Uongozi na Mipango, na Kamati ya ulinzi na Usalama na Uakuu wa Idara wamepata fursa ya kuuliza maswali, kama vile gharama ya kununua mashine ya Hydro Form, nanma ya kutambua udongo unaofaa kwa kufyatua matofali ya aina hii, na uimara wa jengo linalojengwa kwa matofali ya aina hii.
Akijibu maswali haya mtaalam toka JKT amesema: mashine ya Hydro Form ya kufyatulia matofali ya aina hii inagharimu Tsh. 80,000,000/= na jinsi ya kutambua udongo bora kwa ajili ya kufyatua matofali ni kupeleka kiasi kidogo cha udongo maabara jijini Dar Es Salaam kwa ajili ya kupimwa na kutambua kama unafaa. Njia nyingine kuchukua udongo na kuuweka kuganyani kisha mwagia maji, udogo huo ukipitisha maji taratibu na bila kuondoa udogo basi udongo huu unafaa. Pia ameongeza kuwa, majengo yanayojengwa kwa matofali ya aina hii hudumu kwa muda wa miaka 100. Aidha msemaji huyo wa JKT amesema, wako tayari kwa kuwafundisha vijana kwa makundi pale inapohitajika ili kuwepo kwao katika eneo hili kulete matokeo chanya kwa wananchi wanaowazunguka.
Wajumbe wa kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Kamati ya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara wakitembezwa na kuelezewa jengo la Zahanati linalojengwa kwa matofali yaliyotengenezwa kwa kutumia Mashine ya Hydro Form. (Picha Na. Shaibu J. Masasi - Afisa TEHAMA , Mpwapwa)
Kutokana na jengo hili kuwa kubwa wageni hao toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wameshauri zahanati hii kuwa ni kituo cha afya kwa sababu jengo kubwa lenye vyumba vingi vinavyolingana idadi ya vyumba vya vituo vya Afya, pia kwa kuwa zahanati hii inatarajia kutoa huduma zenye hadhi sawa na kituo cha afya.
Mafundi wa JKT wakijenga jengo la Zahanati kwa matofali yaliyotengenezwa kwa kutumia Mashine ya Hydro Form. (Picha Na. Shaibu J. Masasi - Afisa TEHAMA , Mpwapwa)
Aidha uongozi wa JKT umesema tangu kuanzishwa upya kwa kambi hii kumeleta matokeao chanya hasa katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa wananchi wamezuiwa kulima, kufuga, kuwinda na kukata miti katika maeneo yanayoizunguka kambi ya jeshi.
Baada ya kujifunza teknolojia hii na kuuliza maswali mbalimbali na kueleweshwa kwa kina juu ya aina hii ya ujenzi, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amemshauri Mwenyekiti wa Halmasahuri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Donalth Nghwenzi pamoja na wajumbe wote walitembelea JKT kwa ujumla kuwa waanze kutumia teknolojia hii katika miradi ya ujenzi wa majengo ya halmashauri mfano midana ya kisasa, majosho, zahanati, shule na ofisi mbalimbali.
Hata hivyo mwenyekiti Wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa amesema ameupokea ushauri huo na ataufanyia kazi ili kutekeleza miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa
kutumia teknolojia hii ila kufuata taratibu, kanuni na sheria za fedha na vikao vya Baraza la Madiwani. Pia amemshukuru sana Mkuu wa Wilaya na Uongozi wa JKT kwa kuwapatia fursa ya kujifunza teknolojia hii mpya ya ujenzi wa majengo.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (wa tatu kutoka kushoto), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Donalth Nghwenzi (wa pili kutoka kushoto) Kaimu mkurugenzi Mtendaji (W) Ndg. Maria Leshalu (wa kwanza kutoka kushoto) na wajumbe wengine wa kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Kamati ya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara wakiwa katika picha ya pamoja katika Ofisi Kuu ya JKT iliyojengwa kwa matofali yaliyotengenezwa kwa kutumia Mashine ya Hydro Form. (Picha Na. Shaibu J. Masasi - Afisa TEHAMA , Mpwapwa)
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.