(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri amefanya ziara katika kituo cha Afya cha Kibakwe kuona umaliziaji wa majengo ya kituo hicho unavyoendelea. Katika ukaguzi wa majengo yote mkuu wa wilaya ameona ujenzi unavyoendelea na hatua iliyofikia ni ya ukamilishaji tu na mafundi wako kazini. Katika nyumba ya Mganga ujenzi unaendelea na upo katika hatua ya kuwekwa milango.Pia katika nyumba hiyo Mkuu wa Wilaya amepewa maelezo na kamati ya ujenzi kuwa jengo halijafunywa nyaya za umeme (wiring).
Kutokana hali hii ya kutofungwa kwa nyaya za umeme katika nyumba hiyo ya mganga, Mkuu wa Wilaya amelazimika kumtafuta fundi umeme aliyepewa kazi hiyo kutaka kujua kwa nini hajakamilisha kazi. Fundi umeme alipoulizwa kwa nini hajakamilisha kazi, alieleza kuwa alikuwa analipwa kidogo kidogo na mpaka sasa amelipwa Shilingi Milioni ishirini na tano tu pamoja na ufundi. Wakati Mkataba unaonenyesha ni Shilingi Milioni ishirini na tisa tu pamoja na feni na Air condition (A.C). Kwa hiyo feni na AC ameshindwa kufunga kwa kuwa hakupewa fedha kwa ajili ya vifaa hivyo lakini pesa ya vifaa vya umeme na ufundi yote alilipwa.
Nyumba ya Mganga ambayo bado haijafungwa umeme katika Kituo cha Afya cha Kibakwe
Baada ya maelezo hayo ya fundi umeme, Mkuu wa Wilaya amemuagiza Fundi Umeme amalize kazi ya kufunga nyaya za umeme nyumba yote ya mganga kabla ya tarehe 5 Januari, 2019 na atakuja kukagua. Pia Mhe. Shekimweri amemueleza Fundi Umeme huyo kuwa "Serikali imeleta miradi hii kwa Local Fundis ili nao wapate fedha na kuthamini kazi zao nzuri wanazozifanya. Lakini kwa kutokuwa waaminifu kwa baadhi ya mafundi mtasababisha mkose kazi hizi za Serikali". amesema Mhe. Shekimweri.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya amekagua Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) na kugundua kasoro kadha ikiwemo jengo kutokamilika katika hatua za umaliziaji katika milango ambapo mafundi walikuwa wakifunga milango. Pia kuna baadhi ya vigae vya sakafuni (tiles) vimewekwa vibaya, kuna baadhi ya kuta hazijamaliziwa kupigwa plasta wakati jengo lote limepakwa rangi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji Wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul Mamba Sweya (kulia) wakikagua majengo ya Kituo cha Afya cha Kibakwe
Kufuatia hali hii ya jengo hilo la OPD kutokamilika na kuwa na kasoro nyingi, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Shekimweri amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Paul Mamba Sweya kuhakikisha kasoro zote zinarekebishwa na jengo linakamilika kabla ya tarehe 15 Januari 2019, kwa kuwa tarehe hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dtk. John Pombe Magufuli anatarajia kuzindua vituo vyote vya afya nzima na viaze kufanyakazi mara moja.
"Mimi kama Mkuu wa Wilaya ninayemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dtk. John Pombe Magufuli sitokubali kuona vituo vya afya vimezinduliwa Nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma alafu kituo cha Afya cha Kibakwe bado kipo katika ujenzi". amesisitiza Mhe. Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri akikagua nafasi kubwa iliyoachwa wazi katii ya ukuta na tiles jengo la OPD katika Kituo cha Afya cha KIbakwe
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.