Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa Dc.
Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa (CMT) ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu Paul M. Sweya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wamefanya ufuatiliaji wa Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mtera. Fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya Mtera zilitokana na wananchi wa Kijiji cha Mtera kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwajengea kituo cha Afya katika kijiji hicho wakati akitokea Iringa katika Siku ya Mei Mosi 2018. Mhe. Rais Magufuli aliridhia ombi la wananchi hao na ndipo aliagiza fedha zitolewe kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Mtera. Fedha zilizotololewa ni Shilingi Milioni mia nne tu (Tsh 400,000,000/=).
Timu ya Menejimenti na Kamati ya Ujenzi wakiwa katika majumuisho baada ya kukagua majengo yote ya Kituo cha Afya Mtera.
Mnamo mwezi Aprili mwaka 2020 Kituo cha Afya cha Mtera kilianza kujengwa, majengo matano yalianza kujengwa ikiwemo Jengo la Maabara, Jengo la Upasuaji, jengo la mama na mtoto, jengo la Kuhifadhia maiti na Jengo la Mionzi (X-ray), ambapo kutokana na mkataba majengo yote matano yalitakiwa kukamilika mwezi Juni 2020 lakini mpaka sasa hayajakamilika.
Kutokana na kusuasua kwa ukamilishwaji wa Ujenzi wa Kituo cha Afya hicho, Timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imeamua kufanya ziara ya ufuatiliaji ili kubaini sabubu ya kucheleweshwa kwa ujenzi huo.
Katika ziara hiyo Timu hiyo ilibaini kuwa kuna upungufu wa vifaa vya ujenzi kama saruji, milango hakufungwa kwa kuwa haijakamilika kutengenezwa, madirisha kwa baadhi ya majengo hayajawekwa, baadhi ya majengo hayana vigae vya sakafuni (Tiles), mfumo wa maji taka haujakamilika, milango ya jengo la x-ray iondolewe kwakuwa imepinda na iwekwe mipya, madirisha mawili katika jengo la mama na mtoto yalikuwa hayana ubora na hayafanani na mengine kwa urembo (maua) uliowekwa, sinki la kunawia mikono halijawekwa katika ubora unaotakiwa, baadhi ya mafundi wameterekeza kazi.
Timu ya Menejimenti Ikikagua Ujenzi wa Majengo ya Kituo cha Afya cha Mtera.
Baada ya Ukaguzi wa kina Timu ya Menejimenti na Kamati za Usimamizi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Mtera walikaa kikao cha pamoja na ndio Timu ya Menejimenti iliagiza yafuatayo:
1. Fundi Bahati Sanga aliyetoweka katika eneo la kituo kwa sababu ya kudai kuwa anauguliwa ajulishwe kwa barua kuwa akabidhi kazi ikiwa imekamilika ifikapo tarehe 20 Januari 2021.
2. Fundi wa milango na madirisha akamatwe na apelekwe polisi kuhojiwa na ajulishwe ifikapo tarehe 20 Januari 2021 kazi zote ziwe zimekamilika na hakutakuwa na muda wa nyongeza.
3. Mganga Mkuu na Mafundi Sanifu (Technicians) watatu wahamie Mtera na watashirikiana na kamati ya Usimamizi wa ujenzi kwa muda wote mpaka kituo kitakachokamilika ifikapo tarehe 20 Januari 2021.
4. Vifaa vyote vilivyokwisha vinunuliwe ili kazi ikamilike kwa wakati.
5. Mapungufu yote yaliyobainika yarekebishwe ikiwemo madirisha yabadilishwe, milango ibadilishwe, vigae vya sakafuni viwekwe, masinki ya kunawia mikono yarekebishwe.
Fundi Aking'oa Dirisha lenye kiwango cha Chini na lenye urembo tofauti na mengine baada ya Kuamurishwa na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya WiIaya ya Mpwapwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya, ameishukuru Timu ya Menejimenti kwa ziara yao yenye manufaa na kubaini mapungufu hayo, pia amehaidi kwa niaba ya kamati nzima kusimamia kwa dhati na kurekebisha mapungufu hayo ili kituo kikamilike ifikapo tarehe 20 Januari 2021.
Mwisho, Ndugu Sweya aliwashukuru wanakamati ya Usimamizi wa Ujenzi kwa Usimamizi mzuri hadi kufikia hapa japo kulikuwa na changamoto nyingi na hivyo kuwataka kuendelea kujitoa kusimamia Ujenzi wa Kituo hicho kwa kuwa wao ndio watakaonufaika pamoja na wananchi kwa ujumla.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.