Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa leo imeadhimisha Siku ya Usafi Duniani kiwilaya ambapo kwa mara ya kwanza Nchi ya Tanzania imeadhimisha sikuku hiyo ambayo Dunia huadhimisha kila mwaka Septemba 15. Katika Sikukuu hiyo iliyoadhimishwa katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa zimeambatana na kufanya usafi katika mazingira ya Hospitali hiyo. Ndugu Gloria Balegu, Afisa Tarafa ya Mpwapwa Mjini ndio mgeni rasmi katika Sikukuu hiyo ya Usafi Duniani, akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri.
Mgeni rasmi Ndugu Gloria Balegu (wa kwanza kulia aliyesimama) ambae pia ni Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mpwapwa Mjini akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa akitoa hotuba katika Viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Katika sikukuu hiyo Benki ya NMB tawi la Mpwapwa imetoa msaada wa vifaa vya kufanyia usafi kwa Uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, akikabidhi msaada huo Ndugu Beatrice ambaye ni Meneja wa Benki ya NMB tawi la Mpwapwa amesema "Benki ya NMB tawi la Mpwapwa imeona ni vema iungane na Uongozi wa wilaya ya Mpwapwa katika kuadhimisha siku hii ya Usafi Duniani kwa kufanya usafi katika mazingira ya Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa na kutoa msaada wa vifaa vya usafi katika Hospitali hiyo". Aidha meneja huyo ameongeza kuwa Benki ya NMB imekuwa ikitoa misaada mingi ya kijamii kama kusaidia majanga, ujenzi na kuchangia huduma ya afya. Kwa leo Benki ya NMB tawi la Mpwapwa imetoa msaada wa vifaa vya usafi kama vile majembe, reki, mifagio, kwanja na tolori.
Pia meneja wa Benki ya NMB huyo amepata fursa ya kuwatangazia na kuwaelezea wananchi kwa kina kuhusu huduma mpya zinazotolewa na benki hiyo, huduma hiyo ni kama Kukopa pesa NMB ndani ya mwezi mmoja kabla ya mshahara kutoka (Salary Advance) na Akiba kwa wanafunzi.
Mgeni rasmi Ndugu. Gloria Balegu (wapili kulia) akikabidhiwa msaada wa vifaa vya usafi toka kwa meneja wa benki ya NMB tawi la Mpwapwa Ndugu. Beatrice (watatu kushoto) na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya WIlaya ya Mpwapwa Ndugu. Paul Mamba Sweya.
Kwa upande wake mgeni rasmi Bi.Gloria Balegu, akipokea msaada huo toka kwa meneja wa Benki ya NMB tawi la Mpwapwa, amemshukuru meneja wa Benki kwa msaada huo na kuwaomba waendelee kutoa misadaa ya kijamii ili kuinufaisha na kuisaidia jamii ya watanzania.
Vile vile Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ameupongeza uongozi wa benki ya NMB tawi la Mpwapwa kwa kuona umuhimu wa kuungana nasi katika kufanya usafi katika mazingira ya Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa na kutoa msaada wa vifaa hivyo vilivyopokelewa na Afisa Tarafa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya WIlaya ya Mpwapwa Ndugu. Paul Mamba Sweya (wa kwanza kulia) akishukuru Benki ya NMB kwa kutoa vifaa vya Usafi katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa
Mwisho Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari Said Mawji amemshukuru meneja wa NMB kwa kuichagua Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa na kuipatia msaada huo wa vifaa vya usafi, hii inaonyesha kwa jinsi gani NMB imegushwa na masuala ya afya. Kwa ujumla Mazingira safi ni maisha yetu, mazingira safi ni uhai wetu, mazingira safi ni afya yetu, mazingira safi ni uchumi wetu, hivyo kila mmoja wetu ajitafakari namna anavyoweza kuwa na mchango chanya katika kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi. Ikumbukwe usafi ni ustaarabu sharti uanze na mimi.
Kwa taarifa zaidi pakua nyaraka hizi.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.