(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa leo limefanya kikao cha Robo ya Kwanza ya Julai - Septemba Mwaka 2019/2020 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Kikao hicho kilichokuwa kinaongozwa na Mhe. Donati S. Nghwenzi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Massa, kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri, Wabunge, waheshimiwa wa madiwani wa kata 33, wakuu wa idara, watendaji wa kata, maafisa tarafa toka katika taarafa 3 na wananchi hususani wa kata ya Mpwapwa Mjini.
Aidha katika kikao hicho Waheshimiwa Madiwani wameazimia kuwa; eneo la Mazae lipimwe ili kuweza kupata viwanja zaidi ya 1,000 ambapo viwanja hivyo vitauzwa kwa wananchi na hivyo kuiingizia Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa fedha nyingi zitakazotokana na uuzaji wa viwanja hivyo. Pia Maeneo ya Kata ya Mtera yapangwe kwa kufauta hadhi ya mji ili baadae kuweza kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo.
Samabamba na hilo, Baraza hilo limeazimia kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ikamilishe miradi viporo kama vile Zahanati, Mdarasa na Mradi wa Mfereji wa Umwagiliaji katika Kiijiji cha Mafene kata ya Lumuma.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Nghwenzi amewasilisha taarifa yake na kusema kuwa "Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ilipanga kukusanya Tsh. Bilioni 2.2 na kwa robo ya kwanza ya Julai - Septemba 2019/2020 ilipanga kukusanya Milioni 550 na kukusanya mapato halisi ya shilingi Milioni 433 hivyo kushindwa kufikia lengo". Sababu ya kutofikia lengo ni kutoka na hali mbaya ya hewa na kusababisha kupungua kwa mazao ya kilimo, usimamizi hafifu wa vyanzo vya mapato. Hivyo ameagiza kuwa jitihada zifanyike katika kukusanya vyanzo hivi kikamilifu.
Mhe. Nghwenzi, ameorodhesha miradi mbalimbali iliyotekelezwa katka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, ikiwemo miradi ya maji 10 kuwa: Mzase, Iyoma, Kidenge, Seluka, Kingititi, Chogora, Bumila, Mima, Kibakwe na Mpwanila ambapo miradi hii mingi haitoi maji na kufanya adha kubwa kwa wananchi kutafuta huduma ya maji, hivyo ameziagiza mamlaka husika kufuatilia miradi hii na kutatua changamoto zilizopo. Pia ametaja jumla ya fedha zilizotolewa kwa miradi ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ni Shilingi Bilioni 4.29 na zilizotumika ni Tsh. Bilioni 1.348, hivyo zingine bado hazijatolewa shilingi Bilioni 2.84.
Aidha Mhe. Nghwenzi, amewasilisha taarifa ya Vituo vya Afya vya Mima, Kibakwe na Pwaga, ambapo vituo vya Pwaga na Kibakwe vinafanyakazi japo havijakamilika. Kutokana na usimamizi mbovu wa vituo hivyo imepelekea kutokamilika kwa vituo kwa wakati na kusababisha harasa kwa serikali, hii ni kutoka na na kuongezeka kwa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) Kibakwe na Pwaga kumesababisha kuongezeka kwa gharama na kutomalizika majengo kwa kuwa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) hayakuwepo na katika mwaongozo (ramani) uliotolewa na Serikali. Pia ameongeza kuwa Ushauri wa Kujenga jengo la OPD ulitolewa na wataalam wa Halmashauri akiwemo Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya na Mganga Mkuu wa Wilaya.
Waheshimiwa madiwani wakifuatilia kwa makini mjadala na mada zinazowasilishwa katika Kikao cha Baraza la Madiwani Mpwapwa
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri akitoa salam toka Serikali Kuu amesema kuwa "Viongozi wote wa Wilaya tufanye kazi kwa bidii na kwa kushiriana kuanzia Waheshimiwa madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na watumishi wote kwa ujumla" Ameongeza kuwa "Afisa Utumishi unawajibu wa kukaa na watumishi hawa na kujua changamoto zao pamoja na kuwaelekeza kazi zao vizuri na kufuata sheria, ninayasema yote haya kwa kuwa kama watumishi wakiwa wanaishi kwa amani katika mahali pa kazi hivyo usimamizi wa miradi itakuwa inasimamiwa vizuri. Pia naamini kuwa watumishi hawa wanakiu kubwa ya kuongea na mwajiri wao ili waseme mahusiano yanavunjika wapi ili kutatua changamoto zao".
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri (kushoto) akitoa salam toka Serilkali Kuu katika Kikao cha Baraza la Madiwani
Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, amesisitiza kuwa Idara husika kufanyia kazi maazimio yote yaliyotolewa katika kikao hicho cha baraza la Madiwani ili kuweza kuwapatia wananchi huduma zinazostahili.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.