Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa Dc.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa leo limeapishwa katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. katika hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri na Wakuu wa idara na vitengo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Paul M. Sweya. Wajumbe wote wa Baraza hilo leo wamekula kiapo cha kutumikia wadhifa huo kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka huu.
Baraza hilo limepata Mwenyekiti wa Halmashauri Mpya na makamu mwenyekiti mpya, ambapo kwa upande wa Mwenyekiti ni Mhe. George Fuime ambaye pia ni diwani wa kata ya Mpwapwa Mjini na Makamu Mwenyekiti ni Mhe. Maponda ambaye pia ni diwani wa kata ya Luhundwa.
Kwa ujumla Baraza hili limepata madiwani wapya wengi, wasomi na vijana wenye chachu ya maendeleo, ambapo madiwani hao wameahidi kutumikia wadhifa wao kwa weledi na uzalendo mkubwa ili kuleta maendeleo katika kata yao na wilaya kwa ujumla.
Vilevile Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Fuime ameahidi kuliongoza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mpwapwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, pia kwa kutumia hekima na busara.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Ndugu. Sweya ameahidi kushirikiana na madiwani katika maamuzi ya vikao vyenye tija kwa halmashauri na wananchi kwa ujumla.
******Mwisho*******
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.