Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa imezindua rasmi Mpango Kabambe wa Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH) kwa Wilaya hio ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mpango huu wa kimkakati unaolenga kipindi cha mwaka 2024 hadi 2036 unakusudia kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu na jumuishi za maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa wakazi wote wa Wilaya ya Mpwapwa.
Hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dodoma kwa ushirikiano kati ya taasisi isiyo ya kiserikali ya Water For People Tanzania ilihudhuriwa na Henry Chisute Mkurugenzi wa Ubora wa Maji aliyekuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Maji pamoja na wageni wengine mashuhuri.
Miongoni mwa wageni hao ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Dr. Sophia Kizigo, Mkurugezi Mtendaji wa Wilaya ya Mpwapwa, Mkurugenzi Mkazi wa Water For People Tanzania Dr. Happiness Willbroad, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na wadau mbalimbali wa sekta ya WASH kutoka wizarani, ndani ya wilaya na maeneo jirani.
Mpango huu wa WASH wa Wilaya ya Mpwapwa uliondaliwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya taasisi ya Water For People na Wilaya ya Mpwapwa umetengenezwa kama nyenzo muhimu ya kupanga, kuratibu na kutekeleza miradi ya maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi. Lengo lake kuu ni kuboresha utoaji wa huduma kwa kiwango kikubwa, kwa malengo makuu ya kufanikisha upatikanaji wa asilimia 100 wa huduma za msingi za maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi ifikapo mwaka 2036.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mgeni Rasmi alisisitiza umuhimu wa matumizi bora ya maji na utekelezaji wa mpango huu kwa vitendo, akisema:
"Tunakumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji; hivyo, pale maji yanapopatikana, ni muhimu tuyatumie kwa ufanisi. Ni lazima tukubali kutumia teknolojia na mbinu bora zitakazosaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji. RUWASA na Halmashauri ya Mpwapwa wahakikishe mpango huu hautabaki tu kwenye makaratasi, bali utekelezwe kwa vitendo kama sehemu ya kutimiza malengo ya kitaifa" amesema.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.