Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amempongeza Mhe. Rais kwa kuendelea kuimarisha mazingira bora kwa Watumishi wa Umma sanjari na huduma nzuri kwa Watanzania. Hayo yamebainishwa katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya Machi 12, 2025 kwenye Ofisi ya Tarafa Rudi katika Halmashauri ya Mpwapwa.
"Nimshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuimarisha mazingira mazuri kwa Watumishi wa Umma lakini pia kwa Watanzania kupata huduma. Afisa Tarafa ni kiungo muhimu sana kati ya Serikali kuu na Serikali za mitaa, ndio maana dhamira ya Mhe. Rais kuunganisha huduma hizi ni ili ziweze kufanya vizuri kwa Mkoa wetu” Mhe. Senyamule.
Akisoma taarifa ya Mradi huo, Mhandisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bw. Frank Mabubu, amesema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi 150,000,000 ukiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kutolea huduma kwa Afisa Tarafa na kurahisisha utoaji huduma kwa Wananchi.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika eneo hilo baada ya kukagua Mradi, Mhe. Senyamule ametaja malengo mawili makubwa ya ujenzi wa Mradi huo.
“Lengo la majengo haya ya Serikali ni ubora wake ili kutoa mfano kwa wananchi juu ya ujenzi wa nyumba bora lakini pia ni wananchi kupata huduma nzuri katika eneo hili kwa kutatua changamoto zao.
" Tunategemea atakayetumia ofisi hii awe na jambo moja tu la kutatua changamoto za wananchi”. Amesema Mhe. Senyamule.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.