(Na: Shaibu J. Masasi, Afisa TEHAMA - Mpwapwa)
Kamati ya siasa ya Mkoa wa Dodoma ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma Mhe. Godwin Mkanwa leo imefanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Pwaga na Skimu ya umwagiliaji Msagali katika Wilaya ya Mpwapwa. Katika ziara hiyo kamati ya siasa ya Mkoa wa Dodoma imeambatana na Kamati ya siasa ya Wilaya ya Mpwapwa chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Chibwiye, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Jabir Shekimweri, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Donalth S. Nghwenzi na wataalam toka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. na Mkoani Dodoma.
Madhumuni ya ziara hii ni kukagua na kujiridhisha maendeleo ya miradi ya Serikali kama imekamilika na inafanyakazi iliyokusudiwa. Pia kupokea taarifa ya ujenzi wa miradi hiyo ili kujua kama kuna changamoto ili Kamati ya Siasa iweze kutoa ushauri wa namna ya kukabiliana na changamoto hizo ili miradi iweze kufanyakazi. Vile vile kufahamu kuwa thamani ya mradi na fedha iliyotolewa inafanana kwa kukagua vifaa vilivyotumika katika ujenzi kwa kuzingatia mchanganuo wa ujenzi toka kwa mhandisi.
Ziara hii ya Kamati ya Siasa imeanzia katika mradi wa Kituo cha Afya Pwaga kilichopo kata ya Pwaga ambapo taarifa ya kituo imesomwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Dkt. Archard Rwezahura mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma Mhe. Mkanwa. Katika taarifa hiyo imeelezwa kwamba mnamo mwezi Februari 2018 jumla ya Tsh. 500,000,000/= (Milioni mia tano)zilipokelewa toka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Pwaga. Shughuli za ujenzi zilianza tarehe 25/03/2018 na kuhusisha majengo matano tu lakini kwa kuona uhitaji na umuhimu wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), uongozi uliongeza ujenzi wa jengo hili ambalo hakuwa katika mpango na kufanya idadi ya majengo kuwa sita.
Majengo yaliyojengwa mpaka sasa ni kama yafuatayo:-
1. Nyumba ya Mganga/Mtumishi: Nyumba hii imefikia katika hatua ya umaliziaji ambapo mpaka sas badomfum wa umeme, maji safi na maji taka.
2. Wodi ya wazazi: Imefikia hatua ya umaliziaji lakini bado sehemu chache za kuweka vigae, rangi, kukamilisha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka.
3. Jengo la wagonjwa wa nje (OPD): jengo hili limefikia hatua za umaliziaji ambapo kwa sasa bado sehemu chache za kuweka vigae, rangi, kukamilisha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka.
4. Jengo la kuhifadhia maiti: jengo hili limefikia hatua ya umaliziaji ila bado sehemu chache za kuweka vigae, kukamilisha mfumo wa umeme, madirisha maji safi na maji taka.
5. Jengo la upasuaji: jengo hili limefikia hatua ya umaliziaji ila bado kuweka AC, kukamilisha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka shemu ya kunawia kwa ajili ya upasuaji.
6. Jengo la Maabara: jengo hili limefikia hatua ya umaliziaji ila bado sehemu chache za kuweka vigae, rangi, kukamilisha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka, meza za kufanyia kazi (working tables).
Pia Njia ya kutembelea toka jengo moja kwenda lingine (walk ways): msingi umejengwa na nguzo zimesimikwa ila bado kumwaga zege, kupaua na kuezeka. Kiasi cha fedha kilichotumika mpaka sasa katika ujenzi wa kituo cha Pwaga ni Tsh. 509,108,600/= ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imetoa kiasi cha fedha cha Tsh. 9,108,600/= kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya umaliziaji kwa kuwa fedha zilizopokelewa zimeisha.
Katika taarifa hiyo imeelezwa changamoto zilizojitokeza wakati wa ujenzi wa kituo hiki ni kama ifuatavyo:-
1. Ubovu wa miundombinu ya barabara imesababisha kuongezeka kwa gharama za usafirisaji.
2. Upatikanaji wa maji kwa shida kulinganisha na mahitaji ya maji hali iliyolazimu kununua motor na mipira kwa ajili ya kuvuta maji kwenye bwawa.
3. Upungufu wa fedha ya umaliziaji hali iliyotokana na ushiriki hafifu wa jamii kama yalivyokuwa maelewano ambapo jamii ilipaswa kuchangia nguvu kazi kupia usombaji wa mchanga, mawe kokoto na maji.
4. Kuishiwa fedha kwa mafundi kulikosababishwa na kazi kusimama, hivyo fedha ambazo mafundi wangezitumia kwa ajili ya kukamilisha ujenzi zikatumika kwa matumizi mengine
baada ya kazi kusimama. Hii imepelekea mafundi kuendelea na kazi kwa kusuasua.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa ambaye ndio Mkuu wa Msafara wa Kamati ya Siasa Mkoa Mhe. Mkanwa ameagiza "kuwa ifikapo tarehe 28/02/2019kituo hiki kiwe kimeshakamilishwa kwa sababu wenzenu Wilaya zingine mliopata fedha pamoja wameshaanza kutumia na wakina mama wanajifungua na kulazwa". Pia ameongeza kuwa tarehe hiyo 28/02/2019 yeye na kamati yake watakuja tena kukagua na kutoa hatika kwa kamati ya ujenzi.
Kwa nini wenzenu wamemaliza ninyi bado, na fedha imeisha? Amehoji Mhe. Mkanwa. Hapa kutakuwa na ubadhirifu tu, ameongeza. Kufuatia hali hii Mhe. Mkanwa amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa Ndug. Julieth Mtuy kuja kufanya uchunguzi katika kituo hiki kwa kuwa kazi haifanani na fedha zilizotolewa. Pia amewasisitiza Mhe. Mkanwa wananchi wa Kata ya Pwaga kuchangia nguvu, fedha na vifaa vya ujenzi kama vile mawe, mchanga, kokoto na maji ilia kukamilisha kwa wakati kituo hiki.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa amemhakikishia Mhe. Mkanwa kuwa ifikapo tarehe 28/02/2019 kazi hii itakuwa imekamilika, lakini sio hii tu pia na vituo vya Afya vya Mima na Kibakwe, ameeleza Mhe. Shekimweri.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: 0684705551
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.