Na: Shaibu J. Masasi; Afisa TEHAMA - Mpwapwa Dc
Program ya Kuboresha Elimu Tanzania (EQUIP -T) imeizawadia Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa gari la kisasa aina ya Ford Everest SUV yenye namba za usajili DFPA 5945 lenye thamani ya zaidi ya Tsh. 300,000,000/= kwa ajili ya kusimamia vizuri fedha zilizotolewa na program hiyo ya kuboresha Elimu Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
Akisoma taarifa ya mapokezi ya gari hilo katika Kikao cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kilichofanyika tarehe 14/02/2020 katika Ukumbi wa Halmashauri, Afisa Elimu Msingi Ndugu. Mary Chakupewa amesema kuwa "Naomba kutoa taarifa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imepokea gari kwa ajilia ya shughuli ya Elimu Msingi. Gari hilo limeletwa kama motisha kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kupitia Idara ya Elimu Msingi imefanya vizuri katika kuboresha elimu pamoja na kusimamia fedha za program ya Kuboresha Elimu Tanzania (EQUIP-T) kwa usahihi".
Baada ya taarifa hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mhe. George Fuime ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mpwapwa Mjini aliwaomba wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango pamoja na Wakuu wa Idara kwenda kuliona Gari hilo, ambapo kila mjumbe alijionea mwenye gari hilo la kisasa ambalo ni nzima na nzuri.
Mwisho Mhe. Fuime ameipongeza Idara ya Elimu Msingi kwa kufanya vizuri hadi wafadhiri kuona haja ya kutoa motisha ya gari hilo, hivyo ametoa wito tusibweteke tuongeze bidii ili tuweze kupata zawadi zaidi.
Mpwapwa - Dodoma, Tanzania
Anwani: S.L.P 12
Simu: 255 26 2320122/2320
Simu ya Kiganjani: +255 688639341
Barua pepe: info@mpwapwadc.go.tz
Copyright © 2021 Mpwapwa District Council . All rights reserved.